Mtandao wa wanaharakati wanaopigania wanawake kupewa daraja la upadri, umemtangaza mwanachama wake, Lillian Lewis (75), kuwa padri Mkatoliki huko Michigan, Marekani.
Uamuzi huo ambao unauweka mtandao huo katika hatari ya kutengwa na Makao Makuu ya Kanisa Katoliki duniani (Vatican), umefanyika mwishoni mwa wiki baada ya mwanamke huyo kutangazwa kasisi wa kwanza nchini Marekani.
Alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kuhudhuria masomo ya tauhidi (theolojia) katika Chuo Kikuu cha Marquette miaka ya 1960.
Lewis alisema kashfa za karibuni kwenye kanisa hilo na kutengwa kwa baadhi ya watu ni moja ya mambo ambayo yamemchochea kufikiria kupanda kwenye mimbari na kuhubiri.
“Nimedhamiria kuonyesha njia kwa wengine kwamba wanawake tunayo nafasi kubwa ya kuongoza kanisa kama makasisi. Nina mabinti wanne.
Hakuna hata mmoja ambaye anasali kwenye kanisa hilo (Katoliki),” Lewis aliliambia shirika la ABC News.
“Wamekerwa na matukio ya siku za nyuma, kashfa ambazo zimeliandama kanisa … wanasema Ukatoliki umebakia kuwa wa kwangu, si wao.”
Sherehe za upadrisho wa Lewis zilizofanyika Jumamosi, zilihudhuriwa na wageni 200 kwenye eneo la nyumba yake.
Miongoni mwao walikuwa ni viongozi wa dini isipokuwa wale wa Kanisa Katoliki. Lewis ni mwanachama wa mtandao wa Roman Catholic Womenpriests ambao ulianzishwa mwaka 2002 na umekuwa ukitaka ushirikishi, kumjua Kristo zaidi kwenye karne ya 21 …
wenye mtazamo wa kumfuata Yesu kikamilifu kwa kuwahusisha wanawake kama mitume na watu sawa kama ilivyo katika Injili.
Maofisa wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Michigan ambao hawakuhudhuria sherehe hizo walieleza kuwa waumini wake walioshiriki sherehe hizo batili nao watashughulikiwa.
Askofu Paul Bradley wa Jimbo Katoliki Kalamazoo, alitoa tamko kali kupitia mtandao wa WWMT-TV in Kalamazoo, Mich., akieleza kuwa yeyote aliyeshiriki shughuli hiyo hatambuliwi na Kanisa Katoliki.
Mbali ya kuonywa na jimbo hilo, Lewis alisema shughuli hiyo ilikuwa yenye mafanikio na alitarajia kuwa ingepingwa na Kanisa Katoliki. Hata hivyo, alisema licha ya kupewa daraja hilo, hafahamu jukumu ambalo atapewa na kanisa.
Alisema majirani zake na mwanawe wa kiume na mchumba wake, walimuunga mkono baada ya kutambua nafasi ya mwanamke kama kasisi na kusema yuko tayari kuwafungisha ndoa wapenzi hao.
Hilo ni pigo jipya kwa Kanisa Katoliki ambalo kwa siku za karibuni lina kilio cha kutaka mapadri waruhusiwe kuoa huku Papa Francis akieleza msimamo wake kuwa angependa kuendelea kuwa na mapadri waseja.
via>>mwananchi
Social Plugin