Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Geita Joseph Msukuma akiwahutubia wananchi wa Geita juzi |
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Geita Joseph Msukuma amenusurika kupigwa na wananchi wa katoro akiwa na baadhi ya viongozi wenzake na kuokolewa na jeshi la polisi baaada ya kufika kwenye eneo la ujenzi wa vibanda vya serikali ya kijiji hicho na kuamuru waache ujenzi huo.
Tukio hilo limetokea leo majira ya asubuhi akiwa anaelekea wilayani Chato ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya chama ambapo baada ya kufika kijijini hapo alienda kwenye eneo hilo na kuwakuta mafundi wanajenga akaanza kuwazuia huku akisema kuwa
..... “ tangu Jumamosi nilitoa maelekezo ya kusitisha ujenzi huu imenibidi nifike mimi mwenyewe nasema muache mara moja".
Baada ya kufika hapo wananchi waliokuwa eneo hilo walianza kuhamasishana na kusema kuwa......
"Mwenyekiti huyu amezoea kutuburuza watu wa Geita mjini, kwa hapa atuache sisi tuendelee na ujenzi"
Baada ya muda mfupi umati wa wananchi ulikusanyika haraka sana na kumzingira kwa nia ya kutaka kumpiga kwani hawakufurahishwa na kitendo hicho.
Hata hivyo baada ya kuona hali imekuwa tete Msukuma alitoweka na kwenda kujificha kwenye kibanda cha jirani ili kujinusuru asipigwe na umati uliokuwa umekusanyika wakionekana na hasira huku baadhi ya viongozi aliokuwa nao walianza kutoweka katika mazingira ya utata.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Katoro Joeli Mazemle ameulizwa na mwandishi akasema kuwa ujenzi huo unaoendelea hapo umefuata utaratibu wote kuanzia ngazi ya kijiji.
"Tunashangaa Msukuma alipofanya mkutano hapa siku ya Jumamosi akasema kuwa ujenzi huo usitishwe kwa sababu chama kimesema bila kuainisha tatizo ni nini",alieleza mwenyekiti wa kijiji
Juhudi za kumpata mwenyekiti wa ccm mkoa wa Geita hazikuzaa matunda kwa sababu alikuwa anaendelea na ziara wilayani Chato .
Baada ya kuwa amenusurika kipigo , simu yake haikuweza kupatikana ili kujua kwa undani kuhusu sakata hilo.
Hivi karibuni halmashauri ya mji wa Geita wamekuwa na mgogoro baada ya kuzuia ujenzi wa choo cha soko kuu hadi kikahamishiwa nje kidogo ya mji eneo la Nyankumbu huku Msukuma akimwita mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuwa ni mwehu katika mkutano wake wa hadhara wa juzi uliofanyika mjini Geita.
Na Valence Robert- Malunde1 blog Geita
Social Plugin