Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Geita Joseph Msukuma akiwahutubia wananchi wa Geita |
Kati hali isiyo ya kawaida Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Geita Joseph Musukuma ameagiza wananchi warudi katika eneo la Mwekezaji kinyume cha sheria hali iyotafsiriwa kama kuchochea mgogoro wa ardhi.
Mwenyekiti huyo alitoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya soko kuu mjini Geita wakati akihutubia wakazi wa mji wa Geita katika mwendelezo wa mikutano ya chama hicho ya kushawishi wananchi kuhusu muundo wa serikali mbili katika katiba mpya.
Msukuma alitoa kauli hiyo baada ya mwananchi mmoja kutaka kujua mwenyekiti huyo atasaidiaje wananchi hao ili wapate maeneo yao ya kuchimba na kusaga kokoto katika eneo la mtaa wa Nyantorotoro kata ya Kalangalala wilaya ya Geita.
“Naagiza kuwa ,kuanzia sasa hivi wananchi wa Nyantorotoro mrudi katika eneo hilo na endeleeni kuponda mawe na kusaga kokoto kama kawaida na akatayewagusa naomba mnipigie simu ili nimshughulikie ,sisi ccm ndiyo wenye nchi” alisema Msukuma.
Akizungunza na mwandishi wa habari hizi afisa madini wa kanda ya ziwa Haruna Sementa, alisema kuwa mmiliki halali wa eneo hilo la Nyantorotoro ni Majaliwa Maziku na alimilikishwa kwa mujibu wa sheria na kuwa anamiilki kwa leseni ndogo za uchimbaji madini 10 (PM000229238L2) yenye jumla ya hekta zipatazo 42.89.
Mwandishi wa habari amefanikiwa kuona barua iliyoandikwa na Kamishna msaidizi wa Ardhi kanda ya Ziwa iliyosainiwa na H.U.Kitilya ya tarehe 29 Agosti ,2013 kwenda kwenda kwa wananchi wa mtaa wa Nyantorotoro “A” ilisema kuwa ofisi ya Kamishna imejiridhi eneo hilo ni la Majaliwa Paul Maziku na wananchi hao wamelishalipwa fidia.
“Nyaraka zilizowasilishwa zinaonyesha kuwa Ndg.Majaliwa Paul Maziku baada ya kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya wananchi kuanza kuzuia shughuli zake za kupasua na kusaga kokoto alifanya utaratibu wa kuwalipa fedha wananchi 19 zaidi ya fidia stahiki(mikataba imeambatanishwa) kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na jamii inayomzunguka” inataja sehemu ya barua hiyo ya kamishna msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa.
Barua hiyo ilinakirishwa kwa mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Geita na kwa mkuu wa Wilaya ya Geita kwa ajili ya taarifa na utekelezaji wake.
Sehemu ya barua hiyo inashauri Ofisi ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita kutatua kero hizo na ofisi ya kamishna iko tayari kushirikiana nao ili kuzimaliza.
Alipoulizwa kuhusu mgogoro huo,Majaliwa Paul Maziku na kutowalipa fidia wananchi hao,alisema ...
“mimi ninamiliki eneo hili kihalali na nilishalipa fidia kwa wananchi hao,na mkuu wa mkoa aliunda tume ya kuchunguza mgogoro huo na sasa hivi tunasubiri tume hiyo itoe matokeo yake”
“Lakini nashangaa ni kwanini tume ya mkuu wa mkoa haijatoa matokeo ya uchunguzi wake na sasa mwenyekiti wa ccm mkoa anaagiza wananchi waingie kwa nguvu katika eneo hilo na tayari nilishalipa fidia”
Mkuu wa mkoa wa Geita Said Magalula alikiri kuunda tume hiyo na kwamba ilikuwa ikiongozwa na mwanasheria wa mkoa wa Geita na kwamba anasubiri kamati ya ulinzi na usalama ili bwana Majaliwa Maziku apewe ulinzi wa kutosha maana tume yake iligundua eneo hilo analimilki kihalali.
Na Valence Robert- Malunde1 blog Geita