Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MZIMU WA KUANGUSHA GARI LA POLISI WAMTESA OCD GEITA ,AMFANYIA MAMBO YA AJABU MWANDISHI WA HABARI

NB-Picha haihusiani na habari hapa chini
Katika hali isiyokuwa ya kawaida,Mkuu wa polisi wa Wilaya(OCD)ya Geita Busee Bwire,jana aligoma kusalimiana kwa kushikana mkono na mwandishi wa habari hizi kwa kile alichodai anahofia kumpa laana.

Tukio hilo lilitokea kwenye uwanja wa soko kuu la mjini Geita ikiwa ni muda mfupi baada ya mkutano wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita kuanza.

Mkuu huyo wa polisi alikuwa ameongozana na mtu mwingine ambaye haijajulikana iwapo ni askari wa jeshi hilo au la!.

Mara baada ya kukutana uso kwa uso,mwandishi wa habari hizi alinyoosha mkono wake akiuelekeza ulipo mkono wa OCD Bwire ili wasalimiane lakini katika hali ya kushangaza mkuu huyo wa polisi aliukamata mkono wa mtu aliyekuwa naye na kumpa mwandishi.

‘’Si umetaka mkono..shika huu wa mwenzangu mimi wangu sitaki maana naweza kupatia laana ya bure na si lazima ushike mkono wangu ndiyo maana nimekupa wa huyu mwenzangu maana nao ni mkono tu’’alisikika Bwire akimjibu mwandishi wa habari hizi aliyetaka kujua kulikoni.

Haijajulikana kisa cha OCD Bwire kufikia hatua hiyo,hasa ikizingatia kuwa mara kadhaa wanapokutana na mwandishi wa habari hizi wamekuwa wakisalimiana kwa kupeana mikono.

Hata hivyo baadhi ya mashuhuda walidai huenda sababu ni habari iliyoripotiwa hivi karibuni na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo blog hii ya Malunde1 ikihusu mkuu huyo wa polisi kuangusha gari la polisi alilokuwa akiliendesha na kusababisha watuhumiwa 6 kati ya nane waliokuwa ndani ya gari hilo kutoroka.

Mkuu huyo wa polisi Wilaya aliangusha gari hilo la polisi wakati akiliendesha likiwa na watuhumiwa wanane kati yao sita  waliotoroka baada ya ajali hiyo.

Waliotoroka kwenye ajali hiyo ni pamoja na William Michael,Charles Julius,Mussa Mashili,Joseph John,Nelson Raphael na Omari Sued.

Katika ajali hiyo iliyolihusisha gari la polisi lenye namba  PT 1998, askari polisi  waliokuwa ndani ya gari hiyo walinusurika kufa huku mmoja kati yao aking'oka meno mawili ya mbele baada ya  kuacha njia na kupinduka wakati wakitokea kituo kidogo cha polisi Nyarugusu kufuata watuhumiwa.

Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa,gari hilo ambalo huendeshwa na PC Paulo,wa kituo cha Polisi Geita,wakati wakiwa kituo cha polisi Nyarugusu OCD Bwire alilichukua gari hilo na kuliendesha yeye hadi wakati linapata ajali wakielekea Geita mjini.

Ajali hiyo ilitokea  Mei 7 majira ya saa 2 usiku katika kijiji cha Bufunda,Tarafa ya Busanda Wilaya na Mkoa wa Geita.

Aidha kamanda wa polisi mbali na kukiri OCD Bwire kuendesha gari hilo,alitetea kuwa,alifanya hivyo baada ya dereva wake kukaa nyuma ili kuongeza nguvu ya kulinda watuhumiwa hao.

Na Valence Robert- Malunde1 blog -Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com