Kulia ni Bazil Nyakunga ambaye ni mwalimu akiwa na sare za polisi na bossi wake Godlack Mbehale.
MATAPELI washindwa kubaki njia kuu sasa waanza michepuko mipya ni baada ya jeshi la polisi mkoa wa Iringa kumkamata mwalimu aliyejifanya askari akiwa na fullu kombati za jeshi la polisi na bossi wake aliyevalia kiraia ambae pia ni feki na ni mmiliki wa studio eneo la Kihesa mjini hapa.
Upo usemi usemao kuwa usiombe likukute usilo litegemea kukukuta katika maisha yako na ukipenda kudanganya uwe tayari kudanganywa ,hakuna asiyepata kusikia ama kusoma habari kuhusu utapeli unaoendelea hapa nchini kwa watu wa kada mbali mbali na mazingira yanaonyesha matapeli hawa siku zote ni watu wanaopenda wengine yawakute na sio wao na hata kupenda kudanganya na sio kudanganywa kama ambavyo mwalimu huyo Bazil Nyakunga (20) ambae anatuhumiwa kutapeli wazazi wengi Iringa na Morogoro ambao wanataka watoto wao kwenda kusomea uaskari .
Mwalimu Nyakunga akiwa na bossi wake feki Godlack Mbehale (21) walijikuta matatani kwa kukutwa na wasilotegemea kulipata baada ya jeshi la polisi kuweka mtego kufuatia wananchi wengi kufika polisi kulalamikia utapeli huo wa ajira kwa vijana wao katika jeshi la polisi.
Ramadhan Mungi ni kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa alitonya kuwa jeshi lake lilipopata stori hiyo ya utapeli waliweka mtego eneo la Ipogolo ambapo askari huyo feki alikuwa amepiga kambi la kitapeli kwa kuwasanua mavumba wazazi wenye uchu wa watoto wao kuwa mageda (ma Askari).
Alisema kuwa vijana hao ambao mmoja Nyakunga ambae ni mkazi wa Ilula Mtua katika wilaya ya Kilolo mkoani Iringa ni kijana aliyepata kusoma kozi ya ualimu mkoani Shinyanga na kuwa ndie alikuwa akijifanya na askari polisi na muda wote alikuwa akivaa sare za jeshi hilo.
Mungi alisema kuwa kijana huyo na mwenzake wamepata kuwaliza watu wengi sana Iringa na Morogoro na kuwa mtu wa mwisho wamemliza kiasi cha Tsh 900,000 na kuwa njia wanayotumia ni Nyakunga kama askari baada ya kumpata mazazi na mtu mwinye uhitaji na ajira ya polisi amekuwa akipiga simu kwa boss wake Bw Mbehale na kuiweka simu hiyo katika mfumo wa Laudi spika ili mtu anayetapeliwa kupata kusikiliza vema mazungumzo hayo.
“ Nyakunga kama askari feki baada ya kumpata mteja wa kumtapeli amekuwa akiweka simu yake katika sauti kubwa na huyo boss wake amekuwa akisikika akipanga gharama za mtapeliwa kulipia na baada ya kutoa pesa wamekuwa wakiingia mitini kwa kumta ahadi feki….mfano anapopiga simu anajifanya samahani boss naomba maelekezo ya mwisho huyu mzazi /kijana anataka kazi anapaswa kutimiza nini kwa sasa kabla ya kuitwa katika usaili ”.
Hata hivyo kamanda Mungi alisema kuwa ni vema wananchi kuchukua tahadhari juu ya utapeli huo na kuwa kazi za polisi kwa sasa haziingizwi kwa mtindo huo na kuwa jeshi hilo lina utaratibu wake wa kuingiza vijana ikiwa ni pamoja na kuwachucha toka sekondari kwa kujaza fomo huku wale wa elimu ya juu upo utaratibu na wale wanaochukuliwa kwa utaalam wao pia wanautaratibu wao na si vinginevyo.
Alisema kuwa hakuna usaili wa askari unaofanywa mitaani ama wilayani hivyo vijana hao walikuwa wakifanya utapeli na ni vema wananchi kuchukua tahadhari kubwa .
Pia alisema jeshi lake linafanya uchunguzi ili kubaini eneo ambalo matapeli hao walipata sare hizo za jeshi la polisi na mbinu waliyotumia kuzipata sare hizo ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Hata hivyo kwa upande wao matapeli hao walidai kuwa ni kweli wanafanya kazi na ualimu na mmoja na mmiliki wa studio eneo la Kihesa mjini Iringa na kuwa sare hizo walizipata kutoka kwa rafiki yao ambae ni askari polisi aliyewatuma kuzifikisha kwa ndugu yao askari .
Na Francis Godwin,Iringa