Pale afya ya binadamu inapochezewa!! WATOTO WATIBU WAGONJWA,WALIPWA POSHO SHILINGI ELFU MOJA


Uhaba wa watumishi uliopo kwenye hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi umesababisha watoto  kutumika kutibu wagonjwa hospitalini hapo, imefahamika.

Imeelezwa kuwa  vijana  waliomaliza elimu ya msingi wanapewa mafunzo ya muda mfupi kazini ya utabibu ili wajitolee kuhudumia wagonjwa katika juhudi za kukabiliana na ukosefu wa wauguzi na madaktari.

Pamoja na kukosa wafanyakazi, hospitali hiyo inayotegemewa na vijiji vingi ambavyo havina zahanati haijawahi kuwa na x-ray kwa karibu miaka  20 sasa.

Mwandishi wetu aliyetembelea hospitalini hapo alishuhudia vijana 10 wakiwa na  sare za rangi ya kijani  mgomba wakisaidia kutundikia wagonjwa drip, kutoa misaada kwa waliolazwa mawodini, wengine wakideki na baadhi kuchoma takataka zikiwamo za hospitali.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi, muuguzi msimamizi (jina linahifahidhiwa) alisema; “hawa ni vijana walioamua kujitolea baada ya kuona upungufu mkubwa wa madaktari na wauguzi,” alisema na kuongeza kuwa wanafundishwa hapa wakisaidiana na wauguzi na wanalipwa posho kidogo inayoanzia Sh.1,000.

Naye  Katibu wa Afya wa Wilaya ya Ruangwa, Lazaro Msangi, alikiri kuwapo kwa vijana  hao wanaojitolea akieleza kuwa walipatiwa mafunzo ya awali ya utabibu lakini serikali imewanyima fungu la kuwaajiri hivyo kukwamisha ajira za kudumu.

Aliahidi kuwa kuanzia mwezi huu hawatakuwa kazini tena na sababu ya kuwaondoa ni  kutokana na kutokukidhi sifa za utabibu.

“Hawa vijana waliojitolea mwisho wao utakuwa Juni mosi tumepata  wengine  waliofundishwa na Chama cha Msalaba Mwekundu kutoka Dar es Salaam ndiyo watakaofanya kazi kwa kushirikiana na wauguzi wetu,” alisema Katibu wa Afya.

Alifafanua kuwa bajeti ya serikali kwa hospitali hiyo ni ndogo  isiyoweza kutosheleza kuwaajiri wataalamu wenye sifa stahili kwani kwa kipindi cha miaka mitatu hawajapewa fungu la kuajiri wataalamu na watumishi.

Alisema  vijana wanaokuja kufanya kazi ni wale ambao wako kwenye vyuo vya utatibu na hata wakimaliza mafunzo wakiwaomba wabaki hospitalini hapo hakuna  fungu la kuajiri.

“Tumepewa fungu dogo la kuajiri wauguzi watatu  kati ya 54 wanaohitajika  hospitalini  hapo, tutawapeleka maabara maana huko nako hakuna wataalamu wa kupima sampuli za maabara,” alisema. Daktari Mfawidhi wa Hospital ya Ruangwa, Joseph Anga alisema pamoja na changamoto ya wataalamu wa afya katika hospitali hiyo haijawahi kuwa na  x-ray kwa miaka 18. Pia haina wodi ya wagonjwa mahututi, dawa, vitendea kazi wala vifaa tiba.

Alisema kuwa majengo yaliyopo yamechakaa hakuna sakafu, jambo linawalazimisha kumwaga maji kila mara kuondoa vumbi kabla ya kuanza kuwatibu wagonjwa  na wakati mwingine wanatumia maji yasiyo salama.

“Hapa hospitalini  tunategemea maji ya mvua kuoshea vyombo vya maabara, hata vile vya  wodi ya wazazi kwa vile  kwa  ujumla maji ya chumvi tuliyo nayo hayafai kuoshea vyombo vya kitabibu,”alisema.

Alisema kwa mwezi wanapokelewa zaidi ya wajawazito  250 wanaohitaji huduma ya kujifungua.

Hata hivyo, alisema hospitali haina matangi ya kuhifadhia maji hayo zaidi ya  ndoo chache wanazotumia.

Ziara hii iliandaliwa na Chama Cha Wahabari Wanawake (Tamwa), ambacho kinafanya utafiti kuhusu ukatili,  unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Hivi karibuni wabunge wa kikao cha bajeti kinachoendelea walipinga serikali kupunguza Sh. bilion 130.3 katika Wizara ya Afya kati ya Sh. bilioni 753.8 za mwaka wa fedha 2013/14 hadi Sh. bilioni 622.9 kwa mwaka ujao wa fedha.

Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma za jamii ilisema haikuridhika na mtiririko wa fedha za bajeti  hiyo kwa madai kuwa mwaka umefika robo tatu lakini bado fedha hazijapelekwa wizarani.

Hospitali nyingi zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo uhaba wa wauguzi, vifaa tiba na hata matengenezo ya mashine za kusafisha na mionzi pamoja na X-Ray, jambo ambalo linahatarisha maisha ya wananchi.
CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post