Uhaba wa watumishi uliopo kwenye hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi umesababisha watoto kutumika kutibu wagonjwa hospitalini hapo, imefahamika.
Imeelezwa kuwa vijana waliomaliza elimu ya msingi wanapewa mafunzo ya muda mfupi kazini ya utabibu ili wajitolee kuhudumia wagonjwa katika juhudi za kukabiliana na ukosefu wa wauguzi na madaktari.
Pamoja na kukosa wafanyakazi, hospitali hiyo inayotegemewa na vijiji vingi ambavyo havina zahanati haijawahi kuwa na x-ray kwa karibu miaka 20 sasa.
Mwandishi wetu aliyetembelea hospitalini hapo alishuhudia vijana 10 wakiwa na sare za rangi ya kijani mgomba wakisaidia kutundikia wagonjwa drip, kutoa misaada kwa waliolazwa mawodini, wengine wakideki na baadhi kuchoma takataka zikiwamo za hospitali.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi, muuguzi msimamizi (jina linahifahidhiwa) alisema; “hawa ni vijana walioamua kujitolea baada ya kuona upungufu mkubwa wa madaktari na wauguzi,” alisema na kuongeza kuwa wanafundishwa hapa wakisaidiana na wauguzi na wanalipwa posho kidogo inayoanzia Sh.1,000.
Naye Katibu wa Afya wa Wilaya ya Ruangwa, Lazaro Msangi, alikiri kuwapo kwa vijana hao wanaojitolea akieleza kuwa walipatiwa mafunzo ya awali ya utabibu lakini serikali imewanyima fungu la kuwaajiri hivyo kukwamisha ajira za kudumu.
Aliahidi kuwa kuanzia mwezi huu hawatakuwa kazini tena na sababu ya kuwaondoa ni kutokana na kutokukidhi sifa za utabibu.
“Hawa vijana waliojitolea mwisho wao utakuwa Juni mosi tumepata wengine waliofundishwa na Chama cha Msalaba Mwekundu kutoka Dar es Salaam ndiyo watakaofanya kazi kwa kushirikiana na wauguzi wetu,” alisema Katibu wa Afya.
Alifafanua kuwa bajeti ya serikali kwa hospitali hiyo ni ndogo isiyoweza kutosheleza kuwaajiri wataalamu wenye sifa stahili kwani kwa kipindi cha miaka mitatu hawajapewa fungu la kuajiri wataalamu na watumishi.
Alisema vijana wanaokuja kufanya kazi ni wale ambao wako kwenye vyuo vya utatibu na hata wakimaliza mafunzo wakiwaomba wabaki hospitalini hapo hakuna fungu la kuajiri.
“Tumepewa fungu dogo la kuajiri wauguzi watatu kati ya 54 wanaohitajika hospitalini hapo, tutawapeleka maabara maana huko nako hakuna wataalamu wa kupima sampuli za maabara,” alisema. Daktari Mfawidhi wa Hospital ya Ruangwa, Joseph Anga alisema pamoja na changamoto ya wataalamu wa afya katika hospitali hiyo haijawahi kuwa na x-ray kwa miaka 18. Pia haina wodi ya wagonjwa mahututi, dawa, vitendea kazi wala vifaa tiba.
Alisema kuwa majengo yaliyopo yamechakaa hakuna sakafu, jambo linawalazimisha kumwaga maji kila mara kuondoa vumbi kabla ya kuanza kuwatibu wagonjwa na wakati mwingine wanatumia maji yasiyo salama.
“Hapa hospitalini tunategemea maji ya mvua kuoshea vyombo vya maabara, hata vile vya wodi ya wazazi kwa vile kwa ujumla maji ya chumvi tuliyo nayo hayafai kuoshea vyombo vya kitabibu,”alisema.
Alisema kwa mwezi wanapokelewa zaidi ya wajawazito 250 wanaohitaji huduma ya kujifungua.
Hata hivyo, alisema hospitali haina matangi ya kuhifadhia maji hayo zaidi ya ndoo chache wanazotumia.
Ziara hii iliandaliwa na Chama Cha Wahabari Wanawake (Tamwa), ambacho kinafanya utafiti kuhusu ukatili, unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Hivi karibuni wabunge wa kikao cha bajeti kinachoendelea walipinga serikali kupunguza Sh. bilion 130.3 katika Wizara ya Afya kati ya Sh. bilioni 753.8 za mwaka wa fedha 2013/14 hadi Sh. bilioni 622.9 kwa mwaka ujao wa fedha.
Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma za jamii ilisema haikuridhika na mtiririko wa fedha za bajeti hiyo kwa madai kuwa mwaka umefika robo tatu lakini bado fedha hazijapelekwa wizarani.
Hospitali nyingi zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo uhaba wa wauguzi, vifaa tiba na hata matengenezo ya mashine za kusafisha na mionzi pamoja na X-Ray, jambo ambalo linahatarisha maisha ya wananchi.
CHANZO: NIPASHE
Social Plugin