Mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa kwa sababu za maadili) (24) mkazi wa Kijiji cha Omuga, Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara amefanyiwa ukatili wa kutisha wa kusimikwa kijiti sehemu zake za siri na shemeji zake ili kulazimishwa kuhama baada ya mumewe kufariki dunia.
Baba mzazi wa mjane huyo, Alex Allal amesema kuwa mara baada ya kupata taarifa za ukatili huo aliofanyiwa mwanaye aligundua tayari alishatimuliwa kwake akawa anatangatanga na mtoto wake mdogo wa kiume mwenye miaka saba.
Baba huyo alidai amefedheheshwa na kitendo cha shemeji wa binti yake kwa kumpiga kisha kumfanyia ukatili huo.
“Baada ya kufanyiwa unyama huo, tuliripoti polisi na kupewa RB namba UTE/RB/256/2014 na mmoja wa shemeji zake aitwaye Isaya Elphas alikamatwa Mei 28, mwaka huu na wengine kutoweka,” alisema.
Naye mjane huyo alidai kuwa, alianza kunyanyaswa na shemeji zake hao baada ya mume wake Samwel Elphas kufariki dunia mwaka 2012.
Aliyataja manyanyaso aliyoyapata ni pamoja na kudaiwa kuporwa ardhi hekari mbili zilizokuwa na mashamba ya miwa, migomba,mihogo na mahindi alizoachiwa na marehemu mumewe.
Alidai familia ya wakwe zake imemuomba aondoe shauri hilo katika vyombo vya dola ili wajadiliane na kupata suluhu.
Social Plugin