Wafanyakazi zaidi ya 50 wa hotel ya Alfa na Omega ya mjini Geita wamegoma kufanya kazi kwa masaa 22 kwa madai ya kutolipwa shilingi milioni 29 ikiwa ni malimbizo ya mishahara yao tangu mwezi novemba mwaka jana hadi sasa hivi.
Tafrani hiyo imetokea jana asubuhi baada ya kuungana wote na kufunga geti la hotel hiyo wakishinikiza kulipwa mishahara yao ya mda mrefu huku wakiwazuia wateja kuingia na kutoka walioonekana hapo.
Mmoja wa wafanyakazi hao alisema wamekuwa wakifanya kazi kwa mazingira magumu huku wakiwa wanaahidiwa watalipwa mishahara yao kila kukicha jambo ambalo limewaudhi ikawalazimu kuungana kwa pamoja kudai haki yao.
Aliongeza kuwa haki hiyo imesababisha hadi wamefukuzwa kwenye nyumba walizopanga kwa kudaiwa kodi na huku familia zao zikila mlo mmoja hali inayopelekea kushindwa kuendesha maisha yao.
Meneja wa hotel hiyo Costantine Kasembe alipoulizwa kudaiwa kwa malimbikizo hayo alisema...
"Ni kweli mimi nimekuwa nampelekea taarifa mkurugenzi kwa kila kinachoendelea lakini yeye amekuwa hafuatilii".
Kwa upande wa mkurugenzi wa hotel hiyo Andrew Shirima alipoulizwa kudaiwa na wafanyakazi wake alisema kuwa ni kweli wanamdai lakini akaongeza kuwa meneja wake amekuwa hampi taarifa za ukweli kwa sababu anachojua ni kuwa meneja alishampa mamlaka ya kulipa wafanyakazi wote na alikuwa hajapata malalamiko yoyote ya malimbikizo kwa mda mrefu huo lakini akaahidi kuwalipa ndani ya siku kumi.
Hoteli hii ni moja ya kivutio kikubwa katika mkoa huu ambayo imekuwa ikipokea wageni mbalibali wa ndani na nje ya nchi huku baadhi ya wafanyakazi wa mgodi hususani wanaotoka nje ya nchi wamekuwa wakiishi humo.
Na Valence Robert wa Malunde1 Blog- Geita