Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZI WA DAWA ZA BINADAMU KATIKA ZAHANATI,VITUO VYA AFYA,HOSPITALI SHINYANGA WATAWALA,MKUU WA MKOA AFUNGUKA MENGI SOMA HAPA



Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga 


Imeelezwa kuwa nchi ya Tanzania haina upungufu wa dawa za binadamu katika vituo vya afya zahanati na hospitali badala yake kuna wizi wa dawa unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu hali inayosababisha kuongezeka kwa vifo vya mama na mtoto katika jamii kwa kukosa dawa muhimu.

Hayo yamesemwa juzi na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga wakati wa warsha ya siku moja kuhusu mikakati ya kupunguza vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi katika mkoa wa Shinyanga iliyofanyika mjini Shinyanga.

Mkuu huyo wa mkoa alisema hivi sasa limezuka wimbi la wizi wa dawa katika vituo vya afya,zahanati na hospitali hali inayofanya wahitaji wa dawa kukosa dawa hizo matokeo yake wanapoteza maisha.

Rufunga alisema kitendo cha wizi wa dawa kinafanywa na baadhi watumishi wasio waaminifu wasiotaka kuwajibika wenye usimamizi mbovu ambao wanasababisha upotevu wa dawa kwa manufaa yao binafsi.

“Hatuna tatizo la uhaba wa dawa,kinachotusumbua ni huu wizi wa madawa,tumebaini wizi huu,hatukubali kwani hata ukifanya utafiti unakuta dawa za serikali zinauzwa mtaani kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi”.alieleza Rufunga.

Mkuu huyo wa mkoa alisema pamoja na serikali inayoongozwa na rais Jakaya Kikwete kujitahidi kuwahudumia wananchi kwake kwa kuimarisha huduma za afya ikiwemo afya ya mama na mtoto lakini kuna baadhi ya watendaji wasiotaka kuwajibika wanaosababisha hata dawa zisiwafikie walengwa wanaficha dawa za wagonjwa.

Kwa upande wake Daktari kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii Dkt Rutasha Dadi ambaye pia ni anatoka UNFPA aliwataka watendaji na watumishi wa sekta ya afya kuwajibika ipasavyo katika kukabiliana na vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi kwa kuboresha miundo mbinu katika vituo vya afya pamoja na kuhamasisha akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya afya pamoja na kuwaelimisha wananchi wajiunge na mfuko wa afya ya jamii.

Naye mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe  alisema miongoni mwa mikakati ya kukabiliana na vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi katika mkoa huo ni kufungua vituo vyote vya afya vilivyokamilika sambamba na kuandaa mpango mkakati wa kiwilaya na kimkoa wa miaka mitatu wa kupunguza vifo hivyo.

Dkt Kapologwe alisema mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na changamoto ya vifo vya mama na mtoto hivyo kuitaka jamii nzima akiwemo akina baba kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita vifo hivyo kwa kuwahamasisha akina mama kuhudhuria kliniki na kujifungulia na kwenye vituo vya afya.

Kwa upande wao wajumbe wa warsha hiyo mbali na kuunga mkono jitihada za rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete kuanzisha kampeni ya kupiga vita vifo vya mama na mtoto vinavyokana na uzazi pia walieleza kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi katika sekta ya afya wanaotukana wagonjwa na kuficha dawa muhimu.

Wajumbe hao walisema baadhi ya madaktari na manesi wamekuwa wakitumia lugha chafu na wakati mwingine kuwachapa makofi  akina mama wanaofika katika vituo vya afya hususani maeneo ya vijijini na kuwataka wabadilike mara moja kwani vitanda wanavyolazwa wagonjwa ni vitakatifu.

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com