KAMPUNI ya African Barrick Gold Mine Ltd inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Buzwagi wa mjini Kahama mkoani Shinyanga, imetakiwa kuanzisha mashindano ya michezo kuibua vipaji kwa vijana.
Wito huo ulitolewa juzi na Ofisa Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Julius Kambarage katika uzinduzi wa bonanza la soka lililoandaliwa na mgodi huo kwa kuhusisha makundi ya kijamii yanayojishughulisha na ujasiriamali.
Kambarage alisema pamoja na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na kampuni hiyo hadi sasa katika kusaidia jamii, umechukua uamuzi sahihi wa kuanza kukuza sekta ya michezo kwa vijana hasa soka.
“Kila mtu anafurahia kazi za maendeleo za Buzwagi, lakini kwa hatua hii ya kugeukia michezo kwa vijana, mtakuwa mmefanya vema zaidi kwa sababu michezo ni ajira… Nawasihi kama mtaweza anzisheni michuano ya Kombe la Mahusiano ambalo litashirikisha kila kada ya michezo katika kuibua vipaji na kuimarisha uhusiano sambamba na kusaidia ongezeko la ajira kwa vijana,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Amani Sabasaba, ametoa wito kwa vijana kuitumia fursa ya michezo kama chachu ya kujituma zaidi katika kukuza vipaji vyao na kujipatia ajira kupitia sekta hiyo.
Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Bahati Mwambene, kwa niaba ya Meneja Mkuu Filbert Rweyemamu, alisema bonanza hilo linaloshirikisha timu za vijana litatumika pia kuteua nyota wa kuunda timu ya Kahama Buzwagi itakayoshiriki michuano itakayokuwa ikishindanisha migodi inayomilikiwa na Barrick.
Katika mechi ya ufunguzi ya bonanza hilo linalofikia tamati leo, Daladala Utd iliwachapa Timber FC mabao 5-3, huku zote zikionyesha soka ya ufundi.
Na Ali Lityawi -Kahama
Social Plugin