Watumishi wawili wa idara ya Afya katika kituo cha Afya cha Katoro Wilayani Geita Mkoani Geita wamekumbwa na kashfa baada ya kudaiwa kuwatoza fedha wanawake wajawazito pamoja na watoto wadogo kwa ajili ya matibabu kinyume cha sheria na sera ya afya inavyoelekeza .
Watumishi hao ni Janeth Ayoub na Hilda Cosmas ambao wanadaiwa kuwatoza wanawake wajawazito na watoto kwa nyakati tofauti wakati wakiwa katika wodi ya wazazi ya kituo hicho.
Wanawake waliotozwa fedha ni bi Tatu Juma, Witness Majaliwa na Schola Clement.
Wakitoa malalamiko yao mwishoni mwa wiki iliyopita kwa diwani wa Kata ya Katoro Gervas Daud Kabulu walisema walifika katika kituo hicho Julai 14 mwaka huu na kutozwa kiasi cha shilingi elfu kumi na tano( 15,000/=) kwa ajili ya matibabu kwa kila mmoja na shilingi elfu nane(8,000 kwa ajili ya ununuzi wa mipira (gloves).
Mmoja kati ya wanawake hao Bi Schola alisema kuwa alitozwa kiasi cha Tsh 15,000 kwa ajili ya kugharamia matibabu ya mwanae mchanga Asteria Kabodeko wa umri wa wiki mbili(2) ambaye alikuwa amelazwa katika kituo hicho .
Wengine waliodai kutozwa pesa ni bi Lydia Nuhu na Rehema Elias ambao walilazimika kutoa shilingi 23,000/= na watumishi hao waliokuwa zamu katika wodi ya wazazi usiku wa kuamkia Julai 16 mwaka huu .
Bi Lydia alisema alifika katika kituo hicho majira ya saa 9 usiku wa kuamkia Julai 16 katika kituo hicho na kupokelewa na watumishi hao waliokuwa zamu akiwa na mjamzito Neema Elikana na kumpeleka katika wodi ya wazazi ambapo baada kufikishwa ndani ya wodi aliombwa shilingi elfu nane (8,000) kwa ajili ya kununua mpira (gloves).
Aliongeza kuwa kulipokucha alfajiri Julai 16 alitozwa elfu 15 baada ya Neema kumaliza kujifungua na kupoteza fahamu .
Lydia alisema baada ya Neema kupoteza fahamu aliombwa fedha hiyo ili mgonjwa wake aongezewe maji (Dripu) kwa madai kuwa katika kituo hicho maji hayapo na stoo ya dawa imefungwa hivyo alilazimika kutoa fedha hiyo ili kunusuru maisha ya mtoto wake.
Kufuatia malalamiko hayo diwani wa kata hiyo aliamua kumuita Mganga Mkuu wa kituo hicho Dk Alex Gatuku na kumweleza malalamiko hayo ambapo alionyesha kushangazwa na hali hiyo na kuamua kuorodhesha majina ya wanawake wanane (8) waliodai kutozwa fedha wakiwemo wazazi waliojifungua ndani ya siku saba ambao pia walikiri kutozwa fedha na mtumishi wa wakiume ambaye jina lake hali kufahamika mara moja .
Naye mganga mkuu akalazimika kuwaita watumishi wawili waliokuwa zamu usiku wakuamkia Julai 16 katika wodi hiyo na kufanya nao kikao cha dharura mbele ya diwani wa kata hiyo na katibu mwenezi wa chama NCCR Mageuzi jimbo la Busanda Justin Girobi ambae waliambatana na diwani huyo.
Watumishi hao walikiri kuwatoza fedha kiasi cha 23,000 elfu kutoka kwa Bi Lyidia na elfu nane (8,000) kutoka kwa Josephine James na hivyo kuamriwa kuzirejesha kwa akina mama hao waliokuwa ndani ya kikao hicho.
Watumishi hao walipotakiwa kueleza sababu ya kuwatoza fedha akinamama hao walisema lengo lilikuwa ni kutaka kuwasadia kwa kuwa mtunza funguo katika stoo ya dawa anakaa mbali na kituo na kwamba utaratibu wa kuwataka waja wazito kuja na glove na kapeti upo katika kituo hicho wala siyo utaratibu mpya.
“Tuliamua kumueleza ndugu wa mgonjwa Bi Lydia tukaenda kununua kwa mlinzi wa kituo hiki Magoti Kahitila usiku huo kwa kuwa ndiye huwa anatuuzia inapohitajika",walisema.
Hata hivyo utetezi huo ulipingwa vikali na Mganga mkuu wa kituo hicho .
"Nasema ni marufuku kuuza gloves katika eneo hili na kuwatoza fedha wajawzito na watoto ni talia na nyinyi kwanza kabla Mganga mkuu wa Wilaya (D M O ) hajaja,",alisema Gatuku kwa msisitizo.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa wajawazito na watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano wamekuwa wakitozwa fedha pasipo stakabadhi kwa ajili ya matibabu kinyume cha sheria na ukiukaji wa sera ya Afya.
Kufuatia hali hiyo malunde1 blog iliamua kumtafuta kwa njia ya simu yake ya mkononi mganga mkuu wa wilaya ya Geita ( D M O ) Dk Noel Makuza na alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alisema.....
"Nimesikitishwa na hali hiyo na nimepata taarifa hiyo jana kutoka kwa diwani wa kata hiyo na kwamba nimeanza kuchukua hatua na watakaobainika sheria ya itachukuwa mkondo wake’’.
"Asante kwa kunipa taarifa mwandishi najua inauma akina mama na watoto wadogo kutozwa fedha , si utaratibu wetu, lengo letu ni kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii na tayari nimeshatoa maelekezo kwa uongozi wa kituo hicho kuhusiana na tatizo hilo''.
Na Valence Robert-Malunde1 blog-Geita
Social Plugin