Ikiwa ni siku chache tu baada ya mtandao huu wa malunde1 blog kuripoti habari kuhusu Diwani CCM wa kata ya Isulwabutundwe, Maweda Gwesandili na mtendaji wake Sadik Masalu kuiba fedha kiasi cha Tshs. 1,200,000/= za wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu hatimaye zimeanza kurudishwa.
Uchunguzu uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa tayari mtendaji huyo na Diwani wake wameanza kurudisha na hadi sasa wamerudisha Tshs. laki nne na kubakiza kiasi cha Tshs. laki nane kati ya fedha zote walizokuwa wameiba.
Kaimu Mtendaji wa kata hiyo kwa sasa, Joel Nguku alisema kuwa diwani Maweda na Mtendaji wake wameamua kurudisha pesa hizo baada ya vyombo vya habari kuandika kuhusu wizi huo na wananchi kutangaza kuwaburuza mahakani viongozi hao baada ya waanafunzi hao kukosa kwenda shule lakini akaongeza kuwa pesa zilizorudishwa ni ndogo na kiasi walichochukua.
Nguku aliongeza kuwa pamoja na viongozi hao kuanza kurudisha pesa hizo lakini Sadik Masalu ambaye ni Mtendaji amekataliwa na wananchi wa kata hiyo akaomba kuwa pamoja na kurudisha pesa hizo viongozi hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua kali ili liwe ni fundisho kwa viongozi wengine wenye nia ya kuiba pesa za watoto hao.
Alipoulizwa Diwani Maweda kuhusu kurudisha pesa hizo alisema ni kweli yeye alirudisha kiasi cha shilingi laki nne kwani yeye alikuwa amekopa hizo na nyingine zinazobaki anatakiwa arudishe mtendaji wake kwani yeye ndiye aliyechukua nyingi.
"Ndugu Mwandishi, mimi nilichukua laki nne na nilikopa kwa sababu nilikuwa nina shida hizo laki nane anatakiwa arudishe mtendaji wangu kwani yeye alichukua nyingi "alisema Maweda.
Naye mtendaji huyo alipoulizwa lini anarudisha pesa hizo alisema kuwa yeye na diwani walishirikiana kuchukua pesa hizo lakini anashangaa kuona diwani wake anamnamruka na huku walishirikiana kuiba pesa hizo na kuongeza kuwa wote wanatakiwa kuchangia nusu kwa nusu kwani walikula wote na si yeye peke yake kama wanavyodai diwani huyo.
"Mimi namshangaa diwani wangu anasema kuwa mimi nilichukua pesa nyingi na huku tuligawana wote tunatakiwa turudishe nusu kwa nusu sijui kwanini Diwani anawambia wananchi kwamba pesa zote niliiba mimi huo ni uongo" alisema Sadick.
Na Valence Robert-Malunde1 blog-Geita
Social Plugin