IKIWA ni siku chache baada ya mama mmoja kukatwa mapanga na kuuawa na wanaodaiwa kuwa ni watoto wake katika kijiji cha Nyamtundu katika kata ya Busanda wilayani Geita tukio jingine limetokea mjini Geita ambapo mwanamke mmoja ameuawa kwa kucharangwa mapanga kichwani na watu wasiofahamika kisha kutokomea kusikojulikana .
Tukio hilo limetokea jana mnamo saa 2 usiku katika mtaa wa mission kata ya Kalangalala mjini Geita ambapo mama huyo Lidya Kaiche(55) alipatwa na mauti hayo wakati akiwa nyumbani kwake akisikiliza taarifa ya habari akiwa na mwenzake.
Imeelezwa kuwa na mara baada ya kumaliza kusikiliza wakati anaondoka kwenye eneo hilo aingie nyumbani ghafla watu wasiofahamika walitokea kwenye uchochoro kati ya nyumba yake na ya jirani wakiwa na panga ndipo wakamcharanga akapoteza fahamu.
Imedaiwa kuwa kufuatia tukio hilo watu waliosikia kwa mbali walimkuta ameanguka huku akiwa amekatwa panga kichwani ndipo wakaanza kupiga kelele za kuomba msaada zaidi.
Aidha watu waliokutwa kwenye eneo la tukio na waandishi wa habari hizi muda mfupi baada ya tukio hilo walisema kuwa mama huyo ambaye huwa anafanya biashara ya pombe za kienyeji katika mtaa jirani ni muda ambao mara zote anakuwa ametoka kwenye shughuli zake na kurudi nymbani kujipumzisha lakini wameshangaa tukio la ajabu lililompata.
Mashuhuda hao walisema baada ya watuhumiwa kufanya mauaji hayo waliacha panga hapo na kukimbia kusikojulikana.
Kwa upande wa mme wa marehemu Peter Kaiche alisema wakati wa tukio alikuwa ameenda kunywa kahawa mtaa jirani ghafla alifuatwa na mtoto wake Oscar Peter na kumwambia kuwa mama yake ameuawa kwa kukatwa mapanga.
Kufuatia taarifa hiyo Peter Kaiche ndipo alipoenda na kumkuta mkewe akiwa ameuawa kwa kucharangwa mapanga huku akiwa mwenye simanzi kubwa na kudai kuwa yaliyotendeka anamwachia mungu kwani ndiye muweza wa kila jambo.
Kamanda wa polisi mkoani Geita Joseph Konyo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba upelelezi wa kina unaendelea.
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita
Social Plugin