Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HARAMBEE KUCHANGIA UJENZI WA KITUO CHA POLISI NKOME HUKO GEITA YAFANYIKA ,CUF WASUSIA

 Kulia ni mwenyekiti wa CCM,Mkoa wa Geita  Joseph Musukuma akimkabidhi kitita cha fedha kwa kamanda wa polisi mkoa wa Geita joseph Konyo kilichopatikana kwenye harambee ya ujenzi wa kituo cha polisi Nkome juzi


Awali Msafara wa mwenyekiti wa CCM mkoa  wa Geita Joseph Musukuma ukitoka kwenye jengo la kituo cha polisi Nkome kuelekea uwanja wa mpira Nkome  wilayani Geita kwa ajili ya harambee ya ujenzi wa kumalizia kituo hicho
 Mwenyekiti wa ccm mkoa wa Geita joseph Musukuma aliyevaa miwani akijadiliana jambo na RPC Geita Joseph Konyo nje ya kituo kinachojengwa cha polisi Nkome



Kushoto ni Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo,akiwa na cheki ya mil 13,aliyopewa na mwenyekiti CCM mkoa Geita Joseph Musukuma (kulia) kukamilisha ujenzi wa kituo cha polisi Nkome,muda mfupi baada ya harambee iliyofanyika kuchangia ujenzi wa kituo cha polisi cha Nkome kuisha

OCD Geita Busee Bwire kushoto akijadiliana jambo na katibu wa CCM Wilaya ya Geita, wa tatu kutoka kushoto ni mwenyekiti wa ccm mkoa wa Geita Joseph Musukuma kwenye harambee ya ujenzi wa kituo cha polisi Nkome kijiji cha Nkome,Kata ya Nkome Tarafa ya Bugando Wilayani Geita.

Mkuu wa polisi wilaya ya Geita Busee Bwire akizungumza wakati wa harambee ya ujenzi wa kituo cha polisi mkoani Geita-Picha zote na Victor Bariety-Malunde1 blog-Geita


Jumla ya shilingi laki tano zimepatikana katika harambee iliyofanyika katika kijiji cha Nkome,Kata ya Nkome Tarafa ya Bugando Wilayani Geita.

Lengo la harambee hiyo iliyokuwa inaendeshwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Joseph Musukuma ni kuharakisha na kumalizia ujenzi wa kituo cha polisi cha Nkome na kufanikisha dhana ya ulinzi shirikishi kwa jamii katika kata hiyo ambayo imekuwa na matukio mengi ya uharifu.

Katika harambee hiyo,makada wa chama cha wananchi CUF,na viongozi wao walisusia mbali na kuwa kata hiyo ni ngome ya chama hicho hali ambayo ilionyesha mshangao kwa baadhi ya wageni waliohudhuria tukio hilo ambalo halihusiani na itikadi za vyama vya siasa.

Akiendesha harambee hiyo Musukuma  alisema ili kufanikisha dhana ya ulinzi shirikishi na maendeleo ya vijiji na kata ni lazima wananchi wajitambue katika kutoa michango yao ya hali na mali pasipo kuitegemea Serikali.

Musukuma aliyekuwa ameongozana na Kamanda wa polisiMkoa wa Geita,Joseph Konyo,Mkuu wa polisi wa Wilaya hiyo Busee Bwire na viongozi wa CCM Wilaya na
Mkoa,alisifu maendeleo ya kata hiyo akidai kuwa hata kata ya nzera anayotoka yeye haina maendeleo kama yaliyopo kwenye kata ya nkome.

“Nachukua fulsa hii kuwasifuni wananchi wa kata ya Nkome,viongozi wa kata,vijiji pamoja na Diwani wenu kwa maendelo mliyoyafanya kwani ni mfano wa kuigwa tofauti na kata yangu ya Nzera ninakotoka na kama mungu akitupa uhai tarafa nzima ya Bugando ikapewa hadhi ya Wilaya tutaomba makao makuu ya wilya yawe hapa Nkome’’alisema Musukuma na kushangiliwa.

Akisoma taarifa risala kwa mgeni rasmi Afisa Mtendaji  wa kata ya Nkome Francis Kagoma alisema sababu za kuhamasika kujenga kituo cha polisi ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2010,ulinzi na usalama ibara ya 191 kifungu cha E,kinachohimiza kujenga vituo vya polisi kila Tarafa.

Nyingine ni kuvamiwa mara kwa mara na majambazi yenye silaha kali za moto na kusababisha mauaji ya watu na kutishia amani ya wanajamii wa Nkome,na kupelekea watu kupoteza mali zao.

Kagoma alisema katika ujenzi huo ulioanza rasmi mwaka 2010,kwa nguvu za wananchi,walichangishwa 2200 ambapo kiasi cha tshs 13,070,000 huku lengo lilikuwa ni tshs 38,000,000 na kwamba kiasi hicho kilitumika kukusanya mawe,matofali na kuinua boma.

Baadaye wafanyabiashara wa eneo hilo walijitolea kuliendeleza kwa kuinua jengo hilo kutoka usawa wa madirisha hadi kukamilisha boma,na diwani wa kata hiyo Kalema Chiratu alipewa pesa ya mfuko wa jimbo tshs 3,000,000,zilizonunua mabati,halmashauri ya wilaya ilitoa fedha za mrahaba tshs 3,000,000 zilizonunua mbao na kuezeka boma hilo.

Hata hivyo harambee hiyo iliyokuwa na lengo la kupata tshs 48,000,000 ili kumamilisha ujenzi huo ikiwemo nyumba ya mkuu wa kituo hicho,ilipatikana tshs 5,800,000 pekee.

Kutokana na hali hiyo,mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Geita,Musukuma alilazimika kuokoa jahazi kwa kumkabidhi hadharani  kamanda wa polisi cheki ya tshs 13,000,000 ,lengo likiwa ni kuhakikisha kituo hicho kinakamilika na kuhudumia wananchi.

Akikabidhi cheki hiyo,Musukuma aliwataka wananchi wa kata hiyo kuacha ushabiki wa vyama badala yake kujikita katika maendeleo bila kujali itikadi za vyama kwani katika maendeleo,hususani suala la ulinzihalipaswi kuwa na itikadi za vyamavya siasa.

Kauli ya Musukuma ilikuwa inawalenga wananchi na viongozi wa Chama cha Wananchi CUF,ambapo mbali na kata hiyo kuwa ngome ya chama hicho hakuna kada wa chama hicho wala kiongozi wake aliyejitokeza kwenye harambee hiyo iliyokuwa inafanyika katika uwanja wa mpira wa kijiji hicho.

Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo mbali na kumshukuru Musukuma kwa kuendesha harambee hiyo na wananchi waliojitokeza kuchangia,aliahidi kuwakamata waganga wa jadi ambao wamekuwa wakipiga ramli chonganishi na kupelekea kuongezeka kwa mauaji ya vikongwe kwenye Mkoa wake.

‘’Kwa hili wala siwezi kumung’unya maneno,mkawaambie wale waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi kwamba nimetangaza kiama dhidi yao na nitawakamata tu,nitawafikisha mahakamani na kuwatolea ushahidi wafungwe..haiwezekani mauaji ya vikongwe yakaendelea na sisi vyombo vya ulinzi tupo nitawakamata tu’’alisema Konyo.

Na Victor Bariety-Malunde1 blog -Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com