Malunde1 Blog imepiga stori na Emmanuel Samwel Msigwa (aka Dj Msigwa, Super M,Super Msigwa, The dokta ,Mwambaa!) ambaye sasa ni msimamizi wa kituo cha redio Tumaini International 105.7 mhz kilichopo jijini Dar es Salaam, Dj Msigwa ni miongoni mwa Madj waliokuwa karibu kabisa na Juma Migeto enzi za uhai wake.
Dj Msigwa anaeleza alivyomfahamu Dj Migeto
Mwaka 2005 nilipohamia Shinyanga, Juma Migeto alikuwa mmoja kati ya Madj wa mwanza kabisa kufahamiana naye.
Nakumbuka wakati huo alikuwepo yeye na Dj Shebby ambaye alikuwa anapiga Club Butiama, baadaye kwa kuwa mimi nilikuwa radio (Faraja Fm) tukaungana na Dj Mark steve kuiendeleza iliyokuwa TNT.
Wakati huo kulikuwa na ushindani sana wa Ma Dj sema sisi tulikuwa na nafasi kubwa kwa sababu ya Radio.
Juma nilikutana naye kwa mara ya kwanza kwenye mkesha mmoja karibu kabisa na Radio Faraja alimpigia simu Dj Yah Special ( Yahya Mohamed) kuwa akutane na mimi basi tulipokutana ndiyo ukawa mwanzo wa kufahamiana naye ukaribu wetu ukatufanya tufanye kazi nyingi sana mkoani Shinyanga ikiwemo matamasha mbalimbali ya wasanii na hata nyakati za sikukuu mbalimbali.
Ukaribu wetu huo ndiyo uliopelekea kuzaliwa kwa kundi la vijana Ma dj lilikuwa likiundwa na DJ MSIGWA,DJ MIGETO,DJ ASKOFU pamoja na DJ YAH SPECIAL.
Mimi nilikuwa kiongozi wa kundi msaidizi wangu akiwa DJ MIGETO kundi hilo lilikuwa na majukumu makubwa ya kuhakikisha linakuwa moja kati ya makundi bora ya MA DJ mkoani Shinyanga na kanda ya Ziwa.
Pia tulijiwekea lengo la kuwasaidia vijana wenzetu waliokuwa na nia ya kujifunza kazi hiyo na tukafanikiwa kuwalea na kuvumbua vipaji vingi ikiwemo DJ MOSIMO aka DJ MO ambaye alikuwa DJ BORA wa STREIGHT MUSIC mwaka 2013.
Nakumbuka kauli yetu mbiu ilikuwa ni KIPAJI MTAJI tena aliitoa DJ MIGETO na sote ndiyo ilikuwa kila tukikutana tukumbushane kuwa KIPAJI NI MTAJI.
Urafiki na ukaribu huo ndiyo ulifanikisha ndoa yangu mwaka 2008 na kwa upande wa muziki shughuli yote ilisimamiwa na kundi letu la MA DJ ambalo tulikuwa tunaliita SISI DJ'S hata mavazi ya Bibi Harusi yalishonwa na kampuni ambayo Dj Migeto alikuwa anafanyia kazi zake nje ya kundi la SISI DJ'S.
Ukweli lilikuwa ni kundi ambalo lilituweka pamoja sana vijana kwa kuwa tulikuwa tumetimia kila idara, MA DJ huku tukiwa na mmoja kati ya Ma MC bora kabisa mkoani Shinyanga JORAM MAHUGI ambaye sisi tulizoea kumuita 1 KISS.
Baadaye mimi nikasafiri kwenda nje nchini Ujerumani, Dj Askofu na Dj Yah Special wakaenda mikoa ya nyanda za juu kusini mikoa ya Iringa na Mbeya baadaye tukakutana tena jijini Dar es Salaam pamoja baada ya mimi kurudi.
Wakati huo nilifanya kazi mkoani Mtwara(Pride FM) kwa mwaka mmoja, ndipo tulipokutana tukawa na wazo la kuendeleza kundi letu jijini Dar es Salaam kuwa wote sasa tulikuwa tupo.
Juma Migeto alipenda sana tufanye kazi kwa pamoja hakuna vitendo vya kila mtu afanye kazi ki vyake maana aliamini katika umoja na alikuwa mara kwa mara alikuwa anasisitiza turudi Shinyanga ili walau tufanye tamasha moja kwa heshima ya watu wa Shinyanga.
Unajua Malunde,Dj Migeto licha ya yote hakuwa na majivuno hakuwa mchoyo kukuambia kuwa wewe unaweza kitu fulani kwa mfano ni yeye ndiye alinipachika jina la Dokta .
Wakati fulani tulifanya interview ya radio akasema "Msigwa kuanzia leo wewe ni nakupa hadhi ya Udokta na nilipomuuliza akasema mimi mara nyingi nafanya vitu sahihi sana katika kucheza na mashine "
Dj Migeto akawa anasema hajawahi kuona kwa mtu yeyote hasa kwa ma dj kitu ambacho ni ma dj wachache sana ambao wanaweza kukuambia hivyo ndiyo maana kama unakumbuka toka wakati huo ukitaja majina yangu ya aka utasema Dokta.
Kiukweli mimi nimepoteza mmoja kati ya marafiki zangu wakubwa sana katika kazi na yeye ana mchango mkubwa sana katika kazi yangu najua kila ninapotaja aka zangu hasa Dokta huwa namkumbuka sana.
Juma Migeto, hakuwa mgomvi wala mpenda ugomvi pia alikuwa mvumilivu mkubwa sana hata pale tulipofanya kazi kwa malipo madogo kabisa lakini yeye alisisitiza kuwa kipaji ni mtaji na ipo siku tutavuna kikubwa.
Nitamkumbuka sana Juma Migeto na ndoto zake za kutaka turudi tena Shinyanga tufanye walau tamasha moja hazijatimia kwa kweli maana siku za karibuni alikuwa anasisitiza mara kwa mara kila ukiongea naye anakumbusha lini tutaenda Shinyanga Msigwa!!
Ukweli kwa sasa tunajipanga kuja Shinyanga na tutafanya tamasha moja kubwa kwa lengo la kumuenzi Juma Migeto.......
Kwa kifupi mimi nitamkumbuka sana Migeto,namwomba Mungu ampunguzie adhabu za kaburi na raha ya milele amwangazie, hii ni safari yetu sote kaka ameenda akiwa bado kijana tena mpenda maendeleo mapema mno....tumuombee!
Social Plugin