Hatimaye wanachama wa Chama cha Akiba na Mikopo KAGO Saccos cha mjini Kahama wameazimia kuuvunja ushirika huo na kugawana mali baada ya wadau wao kugoma kufanya nao kazi kutokana na ubabe waliokuwa wakiufanya wakati wakiwa kazini.
Uamuzi huo umefikiwa na wanachama hao Julai 14, mwaka huu kwenye mkutano wa dharura uliotishwa baada ya kuibuka mgogoro kati yao na wadau wao ambao ni wamiliki wa mashine za kukoboa mpunga katika Halmashauri ya Mji wa Kahama.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Kago Saccoss John Jonathan aliyowasilisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama Benson Mpesya, ameeleza moja ya sababu zilizosababisha kuvunjwa kwa ushirika huo ni ukosefu wa kazi za uzalishaji kwa wanachama wake.
Amesema chanzo kikubwa cha mapato ya Saccoss hiyo ni wanachama wake kubeba mizigo katika mashine hizo hali ambayo hivi sasa haipo huku kiasi cha Shilingi Milioni 85 zikiwa zimekopeshwa kwa wanachama ambao hawataweza kuzirejesha tena.
Awali Mwenyekiti wa wamiliki wa Mashine hizo Hamisi Mazao amesema wameamua kusitisha mizigo yao kubebwa na Kago Saccoss baada ya kubaini wanachama wake kuwa na lugha chafu kwao ikiwemo kunyanyaswa kwa wateja wao.
Kago Saccoss ilifanikiwa kumiliki jengo la kitega uchumi, pamoja na mtambo wa kuchambua madaraja ya mchele, hivyo kuvunjika kwake ni pigo kwa serikali ambayo iliwekeza zaidi ya Shilingi Milioni 15 zikwemo milioni saba za mfuko wa Jimbo.
via>>Dunia Kiganjani
Social Plugin