Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIJANA AFARIKI DUNIA AKICHIMBA MADINI HUKO GEITA,WANANCHI WAIJIA JUU KAMPUNI YA UCHIMBAJI MADINI KWA UZEMBE WA KUWEKA ULINZI

Wananchi wa kijiji cha Nyaruyeye katika kata ya Nyarugusu  wilayani  Geita mkoani  Geita wamelalamikia  kampuni ya MAWE MERU RESOURCES inayomiliki  eneo  la kuchimba dhahabu katika kijiji hicho  kwa kutoweka ulinzi katika eneo hilo.
 
Malalamiko hayo yamekuja baada ya kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Selemani Mayenza(24) mkulima  kufariki mara baada ya kuanguka  na kutumbukia kwenye shimo akiwa anachimba dhahabu.

Kufuatia hali hiyo wananchi  wamezitaka mamlaka husika kuingilia sakata hilo ili watu wasizidi kupoteza maisha katika eneo hilo.
 
Wananchi hao wamesema awali wakati eneo hilo lilikuwa chini ya mwekezaji Baraka kulikuwa na ulinzi wa kutosha na hakuna mtu aliyekufa kwa kipindi chote hicho  lakini tangu aondoke miezi miwili iliyopita mmiliki wa eneo hilo hajachukua hatua ya kuweka ulinzi mbadala, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya watu na wanyama.
 
Akizungumzia tukio hilo katibu kata wa kata hiyo Thobias Costantine alisema kuwa tukio hilo lilitokea tarehe 22  Juni mwaka huu,majira ya saa 3.00  asubuhi katika kijiji hicho akisema kuwa kijana huyo alikwenda kujitafutia riziki katika eneo hilo kwa bahati mbaya  alitumbukia kwenye shimo lenye  maji hayo na kufariki kwa kuzama.

Aidha alisema alimtaka mmiliki wa eneo hilo awajibike kwa kuweka ulinzi mara moja kabla ya madhara zaidi hayajatokea.
 
'Mimi nashangaa kwa nini huyu mmiliki wa kampuni ya MAWE MERU RESOURCES haweki haharakishi kuweka walinzi katika eneo hili ili kunusuru watu na mifugo",alieleza katibu kata huyo.
 
Afisa madini mkazi wa mkoa wa Geita Haruna Semeta alipoulizwa kuhusu mmiliki halali wa eneo hilo alisema awali mwekezaji alikuwa ni Baraka lakini baada ya kumaliza mkataba wake alirudisha kwa MAWE MERU RESOURCES, ambaye ni mmiliki halali wa eneo hilo na kuhusu kufa kwa watu na mifugo alisema yeye si msemaji wa hilo na msemaji ni mwenye kampuni.
 
Lakini pamoja  na kuhangaika kwa muda mrefu  mwandishi wa habari hizi alimtafuta mmliki halali wa eneo hilo ambaye ni Justin Ernest  katika mahojiano yake kwa njia ya Simu alikiri kumiliki eneo hilo.

 Kuhusu kufa kwa watu na mifugo katika eneo hilo alisema kuwa jitihada za kuweka ulinzi zinaendelea na kuhusu watu kupoteza maisha alisema kuwa mwanasheria wa Kampuni amemuandikia barua muwekezaji wa awali ili aje afukie Mashimo aliyoyaacha.
 
Jeshi la polisi mkoani Geita limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na uchunguzi  kubaini chanzo cha tukio hilo  unaendelea na hakuna aliyekamatwa juu ya tukio hilo.

Na Valence Robert-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com