KIJANA wa miaka 22 Ijumaa alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu katika Kaunti ya Murang’a baada ya kupatikana na hatia ya kuiba jogoo wa familia yao na kisha kumtisha mamake alipomfumania akitekeleza wizi huo.
Bw John Ng’anga alikuwa amefikishwa mbele ya mahakama ya Kandara akikabiliwa na mashtaka hayo na hatimaye akakabidhiwa hukumu hiyo.
Akimhukumu, hakimu mwandamizi wa Kandara Bw Tito Maoga alisema kuwa ni lazima angemtia adabu kijana huyo kwa kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha bila taswishi yeyote kuwa alitekeleza makosa hayo.
“Upande wa mashtaka umefanya kazi ya kufana kuthibitisha kesi dhidi ya mshukiwa. Umeleta hata jogoo aliyekuwa ameibiwa na mashahidi
waliojitokeza ni wa kuaminika na ambao wamehusisha mshukiwa moja kwa moja na wizi huo na kisha kumtisha mamake mzazi aliopojaribu kumzuia kuiba,” akasema.
Kiongozi wa mashtaka Chifu Inspekta Lawrence Wambua alifahamisha mahakama kuwa wiki mbili zilizopita kijana huyo akiwa amejihami kwa rungu aliingia katika chumba cha kuku wa wazazi wake na akaponyoka na jogoo huyo akiwa na nia ya kwenda kumuuza.
“Mamake aliposikia vurugu katika chumba hicho, alitoka nje na akakumbana na mshukiwa akiwa amemuweka jogoo huyo kwa gunia.
Alipomwambia awachane na kuku huyo, mshukiwa alimtisha mamake kwa rungu hiyo ili amwondokee kwa njia,” akasema.
Alifanikiwa kuhepa na jogoo huyo lakini akanaswea njiani akielekea kumuuza sokoni.
Kutafuta kazi
“Chifu wa eneo hilo ambaye alipigia simu madalali kadhaa wa soko alifanikiwa kumnasa kijana huyo alipokuwa anaingia mtaani Kandara kumuuza jogoo huyo. Alikabidhiwa maafisa wa polisi ambao hatimaye walimfikisha kortini,” akasema.
Upande wa mashtaka ulitoa ushahidi kutoka kwa mamake kijana huyo, chifu wake na pia madalali wawili waliomnasa akiwa katika harakati za kumuuza jogoo huyo.
Licha ya kijana huyo kujitetea alikuwa akitafuta pesa za kwenda
kutafuta kazi Jijini Nairobi, Hakimu alimpata na hatia na akamhukumu kifungo hicho huku akitoa onyo kali kuwa kila kijana anayejifunza wizi katika eneo hilo ajitahadhari kufikishwa mbele yake.
“Ukiletwa mbele yangu na hatimaye kesi ikuangukiwe kwa ushahidi usio wa kubahatisha, nitakuondoa miongoni mwa jamii ili ijihusishe na harakati za ujenzi wa taifa bila hofu ya kuhangaishwa na wezi
limbukeni. Tukiwakomesha mkiwa wadogo na mnapojifunza wizi, tutasaidia jamii kuishiwa na wezi sugu,” akasema.
Social Plugin