Kauli ya Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba ya kwamba Tanzania inahitaji kiongozi kijana katika nafasi ya urais mwenye fikra mpya katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015 imechafua hali ya hewa ndani ya chama huku ikipingwa vikali na wanaccm kwa madai kuwa ni ya kibaguzi.
Makamba alitoa kauli hiyo hivi karibuni nchini
Uingereza kauli ambayo imeleta mtafaruku ndani ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi katibu mwenezi
wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga Mjini Charles Shigino alipinga
vikali kauli ya Makamba na kudai kuwa ni kama kuleta siasa za Ubaguzi ndani ya
Chama cha Mapinduzi.
Shigino alisema CCM
inapiga vita suala la ubaguzi wa aina yeyote ile wa binadamu na kuongeza kuwa
kwenye kauli yake hiyo inaweza kuleta hatari kwa mustakabali wa chama na
inaweza kuleta nyufa ya mshikamano wa wanaCCM kwa ujumla.
Aidha Katibu Mwenezi huyo alisema kauli ya Makamba ni
ya kuwabagua wazee kuwa fikra zao hazifai na kwamba kauli hiyo ni kama matusi
ya kiungwana wanayotukanwa wazee hao na alipaswa kuwaomba radhi.
“Namwomba Makamba atambue kuwa ujana sio kigezo cha
kuiongoza jamii ya kitanzania na hasa katika nafasi nyeti ya urais , kisiasa
kijana huyu bado ni mdogo sana ni bora akajifunza kutoka kwa wazee
waliokwishawahi kuiongoza nchi
ambao yeye amekuwa akiwadharau siku hadi siku zinapoenda,”,alisisitiza Shigino.
Aidha Shigino alisema naibu Waziri huyo ni bora
akajipima uwezo wa kuongoza nchi kabla ya kutamani kuwaongoza watanzania hasa katika nafasi ya uraisi katika kipindi cha mwaka
ujao wa uchaguzi.
“Kama kweli Makamba ana nia ya urais ni bora akajipa
muda wa kujifunza na kupata uzoefu wa kutosha wa nafasi ya uongozi katika
nafasi hiyo kwani watanzania wanajua bila
ubishi kuwa katika nafasi ya uongozi ndani
ya Chama cha Mapinduzi hana muda wa mwaka mmoja na nusu”, alisema Shigino.
Mwenezi huyo alisema January Makamba anatakiwa kujua
kuwa Watanzania wanapochagua mgombea uraisi kupitia CCM ndiye huyo huyo
atakayekuwa ni mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi ngazi ya taifa.
Alisema alisema CCM ni Chama kikongwe kina akinamama,
wazee, pamoja na Vijana na anatakiwa kujua kuwa hapo ndipo majawabu ya uzito wa
majukumu yaliopo ndani ya
Chama hicho na Taifa kwa ujumla.
“Mimi pamoja
na wana CCM na watanzania kwa ujumla wenye kulitakia mema taifa kwa ujumla
sioni tatizo la kugombea kijana au mzee au akinamama, suala hapa ni uzoefu wa
kutosha wa kiongozi bila ya kujali tabaka la rika na jinsia”, alisema Shigino.
Pia alisema kuwa kwa sasa Taifa lilipofikia anatakiwa
kiongozi mwenye maamuzi ya kutosha pamoja na uzoefu wa kukabiliana na changamoto
zilizopo za kimaisha ya Watanzania hasa katika nyanja za kiuchumi, Maendeleo ya
jamii pamoja na kisiasa na Utawala Bora.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin