Kufuatia na kukithiri kwa vitendo vya ukatili kwa watoto wadogo kwa kubakwa kisha kutobolewa macho na baadhi ya waendesha baiskeli maarufu daladala,baraza la madiwani la manispaa ya Shinyanga limeazimia kuziondoa daladala zote za baiskeli maeneo ya mjini.
Baraza hilo lilifikia uamuzi huo juzi katika kikao chake cha mwisho wa mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini Shinyanga
Akitoa taarifa ya kamati ya uchumi,afya na elimu mchumi wa manispaa hiyo Christopher Nyarubamba, alisema kamati inashauri kuondolewa daladala hizo katika kata za katikati ya mji na kutakiwa kuwa kando ya mji.
Alisema kamati hiyo pia imependekeza waendesha baiskeli kupatiwa usajili na kupewa vitambulisho ili pindi yanapotokea matukio iwe rahisi kuwabaini.
“Kufuatia kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto,mfano mpaka sasa kuna matukio matano yanayohishwa na waendesha baiskeli hawa,yakihusisha kubaka na ktoboa macho watoto,kamati inashauri
kuondoa daladala zote katikati ya mji,ili kuepuka pia ajali za barabarani”,alisema mchumi wa manispaa.
Kufuatia mapendekezo hayo ya kamati madiwani wote waliunga mkono azimio hilo na kuwataka wananchi wa manispaa ya Shinyanga kubadilika na kuanza kutumia daladala za magari kama ilivyo katika maeneo mengine kwani ni aibu mpaka sasa mji mzima unatumia daladala za baskeli wakati inaitwa manispaa.
Hata hivyo wakichangia hoja hiyo baadhi ya madiwani bi Siri Yasin (CHADEMA) na bi Shella Mshandete (CCM) walisema haiwezekani kuwafukuza waendesha daladala za baiskeli bila kufahamu mbadala wake hivyo kuiomba halmashauri ya manispaa ya Shinyanga iliangalie suala hilo kwa kina japo waliunga mkono kuondolewa kwa daladala hizo.
“Naunga mkono ushauri wa kamati hii,lakini kwanza lazima usafiri upatikane ndipo zoezi la kuwaondoa lianze ,kwani ndiyo tegemeo kubwa la usafiri waliouzoea wananchi hivyo kuwakatisha ghafla italeta tatizo”,alisema Yasin.
“Hili jambo halipingiki ni kweli kuna kero na kuna matukio mengi ya ukatili wa watoto yametokea yaliyosababishwa na waendesha daladala,ni vyema manispaa ikae na wamiliki wa magari kuona namna ambavyo wanaweza kutoa magari yakaanza kusafirisha watu mitaa ya mjini”,aliongeza Shella.
Naye Katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi alisema awali daladala za gari zilikuwepo mjini Shinyanga na uzinduzi ulifanywa na mkuu wa mkoa Ally Rufunga , lakini cha kushangaza wananchi walikuwa hawapandi hali iliyowakatisha tamaa wenye daladala hizo na kuamua kusitisha mpaka sasa na kuendelea kuonekana daladala za baiskeli pekee.
Awali Naibu mstahiki meya wa manispaa hiyo David Nkulila alisema daladala za baiskeli ziondolewe kama lilivyopitishwa azimio,huku akiwanyoshea kidole baadhi ya askari wenye tabia ya kukamata magari ya abiria hovyo wakilenga mitazamo yao ya kimaslahi kuwa halitavumiliwa na kuwataka kuchukua hatua pindi gari linapokuwa na tatizo.
Baraza hilo la madiwani pia lilifanya uchaguzi kumpata naibu meya kwa mwaka 2014/2015 ambapo David Nkulila aliyekuwa anatetea nafasi hiyo kupitia CCM alishinda kwa kura 15 dhidi ya George Kitalama wa CHADEMA aliyepata kura 6.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin