Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KUHUSU MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUWAZUIA MBOWE NA DR. SLAA KUGOMBEA UONGOZI NDANI YA CHADEMA

Msajili wa vyama vya siasa nchini, jaji Francisi Mutungi ameuagiza uongozi wa Chadema kuitisha baraza kuu ili waitishe mkutano mkuu.

Pia, amewazuia mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na katibu mkuu wake Dr. Wilbrod Slaa kugombea uongozi ndani ya chama hicho hadi pale watakapoafikiana kuhusu kipengele cha ukomo wa uongozi.

Uamuzi huo wa jaji Mutungi unakuja siku chache tuu baada ya wajumbe wa mkutano mkuu na baraza kuu wa Chadema kufikisha malalamiko yao kwa msajili, wakilalamikia uongozi wa Chadema kukiuka katiba.

Taarifa ya jaji Mutungi kwa vyombo vya habari, iliyotolewa Dar es salaam, alisema ni vyema wakaitisha mkutano rasmi na halali kwa mujibu wa katiba yao.

Aliongeza, kisha wafanye upya tafakari stahiki kuhusu suala linalohusu marekebisho ya katiba ibara 6.3.2(c), kwa kuzingatia taratibu na hatua zinazopaswa ili kuwezeshwa kwa ibara hiyo katika mkutano mkuu kwa lengo la kupitishwa rasmi na mkutano huo ambao ndiyo wenye mamlaka halali kwa mujibu wa katiba ya Chadema.
 
Kabla ya wajumbe wa mkutano mkuu na baraza kuu kucharuka na kwenda kwa msajili wa vyama vya siasa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba aliwasilisha hoja ya kipengele hicho kwa msajili wa vyama vya siasa.

"Tumekuwa katika mawasiliano kadhaa ya maandishi kuhusu suala linalogusa katiba ya Chadema toleo la mwaka 2006. Mawasiliano yetu yalijikita hasa kwenye hoja ya ukomo wa uongozi kama ilivyo katika katiba yenu toleo la mwaka 2004.

"Kimsingi, Mwigamba kama mwanachama ndiye aliyewasilisha hoja hiyo kudai kuwa, suala hilo limeondolewa katika katiba yao toleo la mwaka 2006, bila idhini ya mkutano mkuu ambao ndiyo wenye mamlaka ya kurekebisha katiba ya chama.

"Ingawa ni kweli mwigamba nimesikia kupitia vyombo vya habari kuwa, si mwanachama wenu tena, lakini yumkini sina shaka hoja inayozungumzwa, bado ni ya msingi, kwa vile inagusa katiba na iliwasilishwa na mtoa hoja akiwa mwanachama wa Chadema,'' alisema jaji Mutungi kwenye maelezo yake kwa Chadema kuhusu yanayoendelea sasa.

Hivyo, wajumbe wa baraza kuu la Chadema na mkutano mkuu walipoamua kwenda kwake wiki iliyopita jijini dar es slaam, aliwaambia malalamiko yao aliyatolea majibu.

Jaji Mutungi alisema barua yake ya januari 15, mwaka huu, alitoa ufafanuzi kuhusu kuondolewa kipengele cha ukomo wa uongozi.

Hivyo, aliamua kutoa taarifa yake tena kwa wajumbe hao ili kuthibitisha kuwa, alishalitolea uamuzi na kuishauri Chadema kuitisha baraza kuu na kisha mkutanao mkuu.

Jaji Mutungi katika barua yake yenye kumbukumbu namba DA.112/123/16A/19, aliwaambia Chadema ni busara hoja ya Mwigamba isiachwe kwa kigezo tu si mwanachama, bali inaastahili kujadiliwa na kupata ufumbuzi wake.

Alisema suala hilo linagusa katiba , hivyo aliamua kulipa uzito unaostahili kwa kuzingatia dhamira tarajiwa ya katiba ya Chadema.

Kwa mujibu wa taarifa ya jaji mutungi ni kwamba,katika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo aliamua kujiridhisha na usahihi wa taarifa hizo kwa kupitia kumbukumbu ilizonazo, ikijumuisha na malezo yao. 

Alisema baada ya kupitia kumbukumbu, ofisi yake ilibaini mambo kadhaa ikiwemola muhtasari wa kikao cha mkutano mkuu wa agosti 13, mwaka 2013 suala la kuondoa ukomo wa uongozi katika katiba yao ya mwaka 2004,halikuonesha kujadiliwa na mkutano mkuu.

Kwa mujibu wa jaji ni kwamba, ibara zilizofanyiwa marekebisho ni 2.4,3.B,4.2.9,5.4.8, 5.4.6, 6.1.1, 6.2.3(d), 7.4B,7.5,7.6,  7.7.5,  7.7.8,7.7.13,7.7.19 na 7.8 kwa maana nyingine hizo ndizo ibara pekee zilizofanyiwa marekebisho na mkutano mkuu wa mwaka 2006.

Pia alisema ibara 6.3.2.(c), ambayo ndiyo mlengwa katika mjadala huo, haikutajwa wala kuonekana katika muhtasari huo.

"Ibara 9.1.3 ya katiba yenu inatajwa kuwa, mkutano mkuu ndio wenye mamlaka ya juu ya kubadili katiba, hivyo suala hilo la marekebisho ya ibara ya 6.3.2(c), budi lingestahili kujadiliwa na kupitishwa kwenye mkutano mkuu''. alisema.

Aliongeza iwapo kama hatua zilizoainishwa kwenye katiba hazikuzingatiwa, vivyo hivyo ofisi ya msajili wa vyama vya siasa hawezi kutambua uwepo, wala matumizi ya ibara hiyo kwa mujibu wa hayo marekebisho yaliyofanyika bila kuzingatia hatua stahiki.

Wakati hayo yanaendelea, kurugenzi ya mawasiliano Chadema kupitia john myika iliweka wazi kuwa, hao wanaojiita wajumbe wa mkutano mkuu wanatumika kuvuruga chama hicho na wakati ukifika, atataja hadharani majina ya wanaofadhili malumbano hayo.

via>>Jambo Leo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com