WATU wawili wamekufa maji papo hapo wakati wakichota maji kwenye dimbwi la maji kwa ajili ya kumwagilia bustani ya mbogamboga, katika eneo la Bunazi lililopo Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Henry Mwaibambe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Jumatano Julai 9, 2014 saa 12.45 jioni.
Katika tukio hilo mama na mwanae walipokwenda kuchota maji katika eneo lililokuwa limejaa maji ambapo mtoto wake aliteleza na kudumbukia ndani ya dimbwi hilo ambapo katika harakati za kumuokoa na yeye aliteleza na kuzama ndani na kupoteza maisha papo hapo.
“Kuna mvua zinazonyesha huku ambazo zilipelekea kuwepo na dimbwi la maji yaliyotuama, sasa wakawa wanalitumia kuchotea maji kwa ajili ya kumwagilia mbogamboga za kilimo ndipo walipozidiwa na maji na kupoteza maisha papo hapo” amesema RPC .
Amebainisha kuwa, katika tukio hilo majirani waliokuwa wanalima kilimo cha mbogamboga karibu na eneo walilokuwa marehemu, waliingiwa hofu baada ya marehemu na mtoto wake kutoonekana kwa takribani dakika 15 ndipo walipofuatilia na kugundua marehemu na mwanae walizama kwenye dimbwi hilo bila kupata msaada na hivyo kuwalazimu majirani kupiga kelele za kuomba msaada. Hata hivyo hawakuweza kuokolewa wakiwa hai.
Amewataja marehemu kuwa ni, Agnes Athumani (25), na Enock Athumani (10) ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Bunazi.
Polisi waliichukua miili ya marehemu baada ya kupata taarifa na kufanya uchunguzi ambapo walikabidhiwa ndugu wa marehemu miili hiyo na kuzikwa leo jioni.
fikrapevu.com
Social Plugin