Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Mauaji tena Kahama!! BIBI AUAWA KWA KUCHARANGWA MAPANGA,AKATWA MIKONO YOTE MIWILI


Mwanamke mmoja aitwaye Milembe Masanja(50) mkazi wa kitongoji cha Muhida kijiji na kata ya Busangi wilayani Kahama mkoani Shinyanga ameuawa kikatili kwa kucharangwa mapanga kichwani kukatwa mikono yote miwili na watu wawili waliokodishwa na familia moja kutekeleza mauaji hayo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi saa mbili usiku.

Kamanda Kamugisha amesema Milembe Masanja aliuawa kwa kukatwa panga kichwani na mikono yote miwili na watu wawili ambao ni Chuchu Lugodisha na mwenzake Ngeja Kugodisha wote wakazi wa kijiji cha Izumba kata ya Luguya mkoani Tabora.

Ameongeza kuwa watu hao walikodiwa na Madaha Luhemeja ili kufanya mauaji hayo huku akitaja chanzo cha mauaji hayo kuwa ni ugomvi wa mipaka ya mashamba kati ya marehemu na familia ya Madaha Luhemeja.

Kamanda Kamugisha amesema kufuatia tukio hilo watuhumiwa wote watatu walikimbia baada ya mauaji hayo na jeshi la polisi linaendelea na msako mkali wa kuwakamata.

Hata hivyo jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu watatu kwa mahojiano ambao ni Pili Paulo(37),Juma Paulo(19) na Daudi Ngassa(57) wote wakazi wa Busangi wilayani Kahama.

Kamanda Kamugisha ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa watu wanaofanya vitendo vya mauaji kwa kukata mapanga baada ya kukodiwa.

Mauaji haya yametokea siku chache tu baada ya bibi mmoja Mkazi wa mtaa wa Nyahanga, wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, Rebeka Sengasenga (82), kuuawa kwa kukatwa na Shoka kichwani kwa kile kilichohisiwa kuwa ni imani za Kishirikina. 

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com