Mshambuliaji wa klabu ya Fluminense ya nchini Brazil Frederico Chaves Guedes Fred usiku wa kuamkia hii leo ametangaza kustahafu kuichezea timu ya taifa lake, ambatyo ilikuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia.
Fred, ambaye hakuonyesha uwezo mkubwa katika safu ya ushambuliaji wakati wa fainali hizo ametangaza kuachana na timu ya taifa ya Brazil akiwa na umri wa miaka 30, huku akiami bado kuna nafasi kubwa kwa wachezaji wengine kushika pahala pale.
Fred, amesema ameamua kuachana na The Canarinho kwa utashi wake binafsi na amewataka mashabiki wake kutodhani lolote katika suala la kushurutishwa kufanya hivyo.
Mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga bao moja katika fainali za kombe la dunia, tofauti na ilivyokuwa wakati wa michuano ya kombe la mabara ambapo alishika nafasi ya pili katika orodha ya upachikaji wa mabao baada ya kuzisalimia nyavu mara tano akitanguliwa na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Hispania Fernando Torres.
Bao pekee alilofunga wakati wa fainali za mwaka 2014, lilikuwa miongoni mwa mabao manne ambapo Brazil ilishuhudiwa ikiiadhibi Cameroon katika mchezo wa hatua ya makundi.
Frederico Chaves Guedes Fred alianza kuitumikia timu ya taifa ya Brazil mwaka 2005 na mpaka anatangaza kustahafu tayari ameshacheza michezo 39 na kufunga mabao 18.
Social Plugin