Aliyeshikilia kipaza sauti ni mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya akizungumza katika uwanja wa taifa Kahama wakati wa African Barrick-Buzwagi Brazuka Bonanza
Serikali ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imeipongeza kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya African Barrick Gold kupitia mgodi wake wa Buzwagi uliopo Kahama kwa juhudi inazofanya katika kubadilisha mji wa Kahama kwa kuwaletea maendeleo wananchi tofauti na maeneo mengine mkoani Shinyanga kama yale yanayozungukwa na mgodi wa Mwadui wilayani Kishapu.
Pongezi hizo zimetolewa juzi na mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya wakati wa kufunga bonanza la soka(African Barrick-Buzwagi Brazuka Bonanza) lililoanza Julai 10,2014 ambapo timu 8 za mpira wa miguu kutoka Kahama zilikuwa zinashiriki mashindano hayo yaliyofikia fainali wakati dunia nzima ikiwa imeelekeza fikra zake nchini Brazil.
Mkuu huyo wa wilaya ya Kahama alisema kampuni ya uchimbaji madini ya Africana Barrick kupitia mgodi wake wa Buzwagi imekuwa mstari wa mbele katika kuibadilisha wilaya ya Kahama kwa kujenga barabara za lami na kusadia katika sekta ya elimu na afya na sasa wamegeukia sekta ya michezo.
Mpesya alisema serikali ya wilaya ya Kahama inatambua ushirikiano mzuri wa mgodi huo na wananchi wa Kahama kwani wameonesha dhahiri kuwa wako pamoja katika kujenga umoja,undugu na ushirikiano katika kufikia hatua ya kufanikiwa pamoja.
“African Barrick siyo wanyama,ni ndugu zetu,nawapongeza pia wananchi wangu kwa kujitoa kushirikiana na African Barrick,tunahitaji ushirikiano huu,tunataka Kahama uwe mji wa mfano mkoani Shinyanga,na baada ya Brazuka Bonanza kutakuwa na Mpesya cup,Jumamosi ijayo,tunataka kila mwisho wa juma kuwe na hekaheka mjini Kahama”,alieleza Mpesya.
“Tunataka kutengeza Kahama inayoenda na wakati,migodi inayotuzunguka inaonesha mfano wa mabadiliko,Buzwagi imejitoa,wamefanya Soka Bonanza,wamekuwepo hapa uwanjani tangu kombe la dunia lianze walikuwa wanaonesha mechi zilizokuwa zinachezwa Brazil”,aliongeza Mpesya.
Kwa upande wake kaimu meneja mkuu mgodi wa Buzwagi Amos John alisema lengo la mashindano hayo kwa vijana wa Kahama ni kuonesha kuwa African Barrick ikom pamoja na wananchi wa Kahama katika kuimarisha umoja,undugu,ushirikiano na mshikamano ili kufanikiwa kwa pamoja katika maisha.
John alisema kuwa katika mashindano hayo jumla ya timu 8 za mpira wa miguu zilikuwa zinashiriki,ambazo ni Afya fc,Bodaboda fc,Timba fc,Daladala fc,Halmashauri ya mji Kahama,Stand fc,Wasanii fc na Bajaji fc,ambapo timu zilizofika fainali ni Afya fc na Bodaboda fc,hadi mwisho wa mchezo Bodaboda fc 3,Afya fc 1 kwa penati baada ya kutoka 2-2 katika dakika 90.
Alisema mshindi wa kwanza katika Soka Bonanza ni Bodaboda fc ambao waliondoka na shilingi laki 5 na mpira mmoja kama zawadi,washindi wa pili ni Afya fc ambao waliondoka na shilingi laki 2 na mpira mmoja na mshindi wa tatu ni Daladala fc ambao walipata shilingi laki 1 na mpira mmoja,huku mechi zingine zilizoshiriki zikiambulia mpira mmoja kila timu.
John alisema Soka Bonanza ilikuwa imeambatana na michezo mingine kama vile kukimbiza kuku na kukimbia kwenye magunia ambapo washindi walipewa zawadi na African Barrick Gold.
Hata hivyo burudani haikuishia hapo wakazi wa Kahama walishuhudia pia fainali za kombe la dunia zilizokuwa zinaoneshwa na African Barrick katika uwanja wa taifa Kahama ambapo pia wasanii walinogesha Brazuka Bonanza akiwemo Ney wa Mitego na Christian Bella na wasanii wengine wa Kahama.
Na Kadama Malunde-Kahama
|
Social Plugin