Mtoto Ismail Mrisho (4) amefariki dunia baada ya kubembea kwenye waya wa umeme uliokuwa umekatika, eneo la Kigogo, jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alithibitisha tukio hilo.
Alisema mtoto huyo alikutwa na mkasa huo jana, majira ya saa 2:30 asubuhi, wakati akicheza nje kidogo na nyumbani kwao.
“Waya wa umeme ulikuwa umekatika na kuning’inia.
Ndipo mtoto huyo aliyekuwa akicheza karibu na eneo hilo pasipo kuonekana na mtu aliushikilia ili abembee bila kujua.
Akanaswa na kufariki dunia papo hapo,” alisema Kamanda Wambura.
Aliwataka wazazi kuwa makini na watoto wao kwa kuhakikisha wanawawekea uangalizi wa kutosha, hasa wanapokuwa mbali na majumbani mwao ili kuwalinda na majanga, ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kwenye jamii.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi na upelelezi unaendelea juu ya tukio hilo.
Social Plugin