NB-Picha haihusiani na tukio katika habari hapa chini |
Mwalimu Festo Twange, aliyeshambuliwa kwa mawe akituhumiwa kuua mwanafunzi kwa kumchapa viboko, amehadithia jinsi mkasa huo uliotaka kutoa uhai wake ulivyo mpata.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, mwalimu huyo alisema siku ya tukio alitoka nyumbani kwake akiwa amechelewa kwa sababu alikuwa akimhudumia ndugu yake mgonjwa katika hospitali ya serikali ya Somanda mjini Bariadi.
Alisema alifika shuleni akiwa amechelewa na kusaini kitabu cha maudhurio na kisha kwenda moja kwa moja darasa la sita kufundisha somo la hisabati.
Alisema akiwa darasani ghafla alifuatwa na walimu wenzake na kuambiwa kuwa anatafutwa na Sungusungu kwa madai ya kumcharaza viboko mwanafunzi wake na kusababisha kifo chake alipofika nyumbani.
Huku akionyesha hali yake kuendelea vizuri hospitalini hapo, alisema baada ya kupata taarifa hiyo alikimbilia ofisi ya Mwalimu Mkuu kwa lengo la kujificha kunusuru adhabu za walinzi hao.
Alisema pamoja na mbinu hiyo bado hakufanikiwa kwani walimwona na kumfuata ofisi ya Mwalimu Mkuu na kuvunja mlango na kuanza kumshambulia kwa silaha za jadi, fimbo, marungu na mawe na kujikuta amepoteza fahamu.
“Baada ya kumaliza kufundisha nilishangaa walimu wakija wanakimbia na kuniambia natafutwa na Sungusungu kwa madai ya kumchapa mtoto na kumuua hali ambayo ilinifanya nijifiche katika ofisi ya mwalimu mkuu..lakini walivunja mlango na kuanza kunishambulia ambapo nilipoteza fahamu na kujitambua nikiwa hapa hospitalini” alisema Twange.
Alisema anachokumbuka ni kipigo kikali na mayowe na baadaye kujikuta akiwa yuko hospitalini huku kichwani akiwa amejeruhiwa vibaya.
Akisimulia zaidi mwalimu huyo alisema kuwa, siku hiyo mwanafunzi huyo Shilinde Ng’holo (12) ambaye sasa ni marehemu hakufika shuleni hapo na wenzake walipoulizwa na mwalimu akiwamo kaka wa binti huyo, alidai mdogo wake amemuacha nyumbani kwao akiwa amelala.
“Shilinde siku hiyo hakufika shuleni hata kwenye mahudhurio ya wanafunzi hakuwapo ambapo na nilipo wauliza wanafunzi wenzake na hata kaka yake alieleza amemuacha nyumbani amelala” alisema mwalimu huyo.
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia watu saba kwa tuhuma ya kuhusika katika tukio la kumshambulia mwalimu huyo, wakiwamo makamanda wa Sungusungu ambao waliokwenda kumkamata mwalimu huyo.
Na ANCETH NYAHORE-simiyu
Social Plugin