Mwanafunzi wa darasa la kwanza wa shule ya msingi Galanzala wilayani Iramba, amekufa papo hapo baada ya kugongwa na mkokoteni wa kuvutwa na ng'ombe, uliokuwa ukiongoza na baba yake mlezi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ajali hiyo ni ya juzi saa 3:00 asubuhi katika kijiji cha Uwanza wilayani Iramba.
Kamwela alisema mkokoteni huo, ambao ulikuwa ukiongozwa na baba mlezi wa mtoto huyo, Samwel Napegwa ulikuwa umepakia miwa kutoka kijiji cha Galanzala na ulipofika kijijini hapo ulimgonga mwanafunzi huyo wakati akijaribu kudandia nyuma.
Alisema kuwa baada ya mwanafunzi huyo kushindwa kudandia kikamilifu, aliteleza kisha kuingia kwenye uvungu wa mkokoteni huo na hivyo kukanyagwa hadi kifo chake.
Kamwela alisema uchunguzi wa awali, unaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa mwongoza mkokoteni huo, ambaye alishindwa kumzuia mwanafunzi huyo kudandia mkokoteni.
Kamanda huyo alisema Napegwa alitoroka na kukimbilia kusikojulikana baada ya kutokea ajali hiyo.
Social Plugin