Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, maarufu kama “Mr. Sugu” amesema ataendelea kupiga mtu ngumi bungeni kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kumsakama wakati akiwakilisha matatizo ya Watanzania ili yapatiwe ufumbuzi.
Alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mashujaa, mjini Mafinga, Wilaya ya Mufindi, katika moja ya siku 72 za ‘Operesheni Tokomeza.
Mbilinyi alisema kama wabunge wa CCM wakiendelea na kumzodoa wakati akiwakilisha matatizo ya watu wake, basi hana budi zaidi ya kuchapa watu makonde bungeni.
“Sugu yupo kwa ajili ya kutetea wanyonge kwa kuwakilisha matatizo yao bungeni ili yapatiwe suluhisho. Sasa nasema hivi, nitakapokuwa nawakilisha mawazo ya wanyonge, halafu wakanizingua, nitaendelea kupigana tena na tena bungeni. Nitapiga watu ngumi huko,” alisema Mbilinyi, huku mamia ya watu wakishangilia.
Alisema jina lake la ‘Rais wa Mbeya’ na kusema alipewa na wananchi wake na hakujipa yeye kama baadhi ya watu wanavyosema.
“Baada ya kuitwa rais wa Mbeya, watu wa usalama wakaanza kunifuata sana wakisema kwanini nautenga mkoa wa Mbeya na kuifanya Mbeya ijitenge na kuwa nchi, lakini mimi sikujipa jina, hili bali watu walisema wewe ndiyo rais wetu, na mpaka leo mimi ndiye rais wa Mbeya,” alisema.
Alisema Mbeya ya sasa siyo ile ya zamani, ambayo vijana walikuwa ‘wakipiga nondo’ na matukio mengine ya kihalifu, bali vijana wake wa sasa ni wale, ambao wanafuata sheria na kanuni za nchi.
via>>Nipashe
Social Plugin