Imeelezwa kuwa sekta ya pamba nchini inaendelea
kudorora kunatokana na wataalamu kutojua uwazi na ukweli wa ujuzi,uzoefu na
hali halisi inayowakabili wakulima ambao wameamua kuwa wakimya hawajui nini
kinaendelea huku viongozi wa serikali wakipewa taarifa ambazo siyo sahihi.
Hayo yamesemwa juzi na mlezi wa chama cha wakulima wa
pamba nchini na msemaji wa wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima zao la
pamba nchini,mbunge wa Maswa Magharibi kupitia Chadema John Shibuda wakati wa
kongamano la siku moja la wadau wa pamba mjini Shinyanga lililoandaliwa na
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania(MVIWATA).
Kongamano hilo lililokutanisha wadau wa pamba kutoka
mikoa ya Mara,Simiyu,Geita na Shinyanga lililenga kujua na kupata ukweli juu ya
kile kilichotokea kuhusiana na mbegu mpya ya pamba UK91(zenye kipara)
iliyozalishwa na kusambazwa na kampuni ya Quton ambapo mbegu hizo hazikuota
vizuri na kuwaletea hasara kubwa wazalishaji wa pamba.
Shibuda alisema sekta ya pamba inazidi kudorora kwa
sababu ya wasomi na wataalamu kufikiria kwamba wao ndiyo wanaojua zaidi hali
halisi iliyopo katika sekta ya pamba huku wakulima wakisahaulika na kuonekana
hawajui lolote wakati wanauzoefu wao tangu enzi za mababu zao.
“Kutokana na ombwe la kutokuwepo uwazi na ukweli wa
hali halisi katika sekta hii panazaliwa visilani vya kusigana kati ya wakulima
na utendaji wa serikali,hii ni kasoro kubwa sana wataalam hawatoi taarifa kwa
uwazi na ukweli”,alisema Shibuda.
“Viongozi hawapewi taarifa zenye uwazi,matatizo haya
ndiyo yanayosababisha mkuu wa mkoa anapewa taarifa ambazo siyo sahihi,anatoa
maagizo ambayo yana kasoro,mkuu wa wilaya naye anagundua maagizo niliyopewa
yana hitilafu,mtiririko huo unakwenda hadi kwa waziri mkuu naye anatoa maagizo
yenye kasoro kutokana na kutopewa uwazi na ukweli”,aliongeza mbunge Shibuda.
Shibuda aliwataka wataalam kuwa makini na kuwataka
wanyumbulishe mazingira ya wakulima na wanapotoa taarifa kutoka serikali kuu kwenda
kwa walengwa mfano wakulima ama wananchi wa ngazi za chini wawe wawazi ili
kuepuka migongano isiyokuwa ya lazima kati ya serikali na wakulima.
“Mtakosanisha serikali na wakulima,na wabunge
hawatakubali,sasa mtaanza kusigana wabunge na serikali,serikali ya CCM,wabunge
wa CCM,maana yake nini sasa,hatumtendei haki mkulima kwani wanaozungumza kuhusu
matatizo ya wakulima wanazungumza kwa lugha rahisi tu,ukweli ni kwamba hizi
mbegu za UK91 zina kasoro”,alisisitiza Shibuda.
Aliwashauri kufanya mnyumbuliko kutambua uzoefu wa
wakulima
Naye mwenyekiti wa MVIWATA mkoa wa Shinyanga Charles
Yona Ndugulile alisema MVIWATA na wadau mbalimbali wa maendeleo vijijini
wanatambua changamoto zinazomkabili mkulima wa pamba na wamekuwa wakifanya
juhudi za kutafuta ufumbuzi wake na sasa wamejielekeza kwenye mbegu ya UK91
kutoota vizuri ili kujua hatma ya wazalishaji walioathirika na mbegu hiyo.
“Zao la pamba ama dhahabu nyeupe kama wengine
wanavyooita,inalimwa katika wilaya zaidi ya 40 katika mikoa 13 ya Tanzania bara
likiajiri wakulima wanaokadiriwa kufika 500,000,thamani yake inashuka kila
kukicha na sasa mbegu ya UK91 ambayo imeleta mitazamo tofauti katika jamii
wengine wanazisifu wengine wanasema hazifai ndiyo changamoto kwa
wakulima”,alieleza Ndugulile.
Akizungumza katika kongamano hilo kaimu mkurugenzi wa
bodi ya pamba nchini Gabriel Mwalo aliwataka wakulima kubadilika na kuanza
kilimo cha mkataba ili kutatua changamoto katika zao la pamba huku akiwataka
kuacha kulima kwa kuangalia msimu uliopita alipata hasara au la.
Alisema sababu zilizopelekea kutoota kwa mbegu isiyo na
manyoya(UK91) kufuatia utafiti wao,mapungufu yapo katika mfumo wa
uchambuaji,uchakataji,utunzaji na usafirishaji wa mbegu kabla ya kumfikia
mkulima na kwamba kuna mbegu zilikutwa na ukungu/fangasi huku wakulima
wakitajwa kukosa elimu sahihi juu ya mbegu hizo.
Kwa upande wake Joseph Ngura kutoka taasisi ya
kudhibiti ubora wa mbegu nchini (TOSCI),iliyohakiki kuwa mbegu zenye
kipara(UK91)zina ubora aliwashauri wakulima kufuata sheria za mbegu kwa kuepuka
kuchanganya mbegu wanapolima kwani zinasababisha ubora wa pamba kushuka.
Naye mkulima kutoka mkoani Mara bwana Godfrey Mukiri
aliomba wakulima waliopata hasara katika msimu wa uzalishaji 2013/2014 walipwe
fidia huku akishauri mbegu ya UK91 iliyopigiwa debe kwamba ina ubora isitumike
tena bali itafutwe mbegu nyingine nzuri pamoja na serikali kuona umuhimu wa
kujenga viwanda vya nyuzi na nguo ili kuepuka kuuza pamba nje ya nchi.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin