Mtu asiyefahamika anayesadikiwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa wa ujambazi, amelimiminia risasi basi la Jeshi la Magereza na kuwajeruhi askari wawili na mahabusu mmoja.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 7:50 mchana, maeneo ya Regency (TMJ) karibu na kwa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam wakati basi hilo likitoka Mahakama ya Mwanzo Kawe kwenda Mahakama ya Kinondoni kuchukua mahabusu wengine.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camilius Wambura, jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo baada ya mtu huyo asiyejulikana kulimiminia risasi kadhaa basi hilo kwenye vioo vya pembeni na nyuma.
Alisema basi hilo lenye namba za usajili MP 0046 aina ya Isuzu lililokuwa na mahabusu lilikuwa likielekea Kinondoni kukusanya mahabusu kutoka maeneo ya Kawe, na baadaye lingewapeleka katika Gereza la Segerea lililopo Manispaa ya Ilala.
"Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kuna mtu alikuwa na bunduki amerusha risasi ndogo ndogo kama za kuulia ndege, zimevunja vioo vya upande wa kulia na kioo cha nyuma,” alisema.
Wambura alisema katika tukio hilo askari Magereza mwenye namba A 9716 Sajenti Msofe, alijeruhiwa kiganja cha mkono wa kulia, askari Polisi wa kike mwenye namba WP 4481 Koplo Dotto wa Kituo cha Polisi Kawe titi la kulia na mahabusu Doreen Damian alipata michubuko kwenye paji la uso na bega la kulia.
“Majeraha yote hayajatokana na risasi bali mabaki ya risasi na vipande vya vioo, walipata matibabu ya awali kwenye Hospitali ya TMJ na baadaye dereva aliendelea na kazi na askari polisi na mahabusi walipelekwa hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu zaidi,” alisema Kamanda huyo.
Hata hivyo, Wambura alipotakiwa kufafanua zaidi aina ya risasi iliyotumika, alisema kitaalamu ni risasi ndogo na kwamba hawezi kufafanua zaidi.
“Hatutajua chanzo, tunachunguza kujua ni nini kilikuwa kinafanyika na dhamira ya aliyerusha risasi hizo, hatujamkamata…hakuna mahabusu aliyetoroka wala kutoroshwa, tunachunguza kwa kina,” alisisitiza.
Wambura alisema pia wanachunguza ili kujua lengo la mfyatuaji wa risasi hizo kama ilikuwa ni kutorosha maabusi au la.
Mmoja wa wauguzi wa hospitali ya TMJ ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema askari aliyejeruhiwa katika titi la kulia amepelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Shuhuda wa tukio hilo alidai aliwaona majambazi wakitokea kwa Nyerere wakikimbia kwa miguu kisha kulishambulia basi hilo lililokuwa mbele yake ambako lilikuwa likisindikizwa na gari la polisi kisha wakatokomea huku mahabusu wakishangilia.
via>>nipashe
Social Plugin