Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA WAPEWA PESA KUJIEPUSHA NA VISHAWISHI VYA NGONO WILAYANI KAHAMA


Baadhi ya vijana hao waliopatiwa pesa
Mkurugenzi wa HUHESO FOUNDATION Juma Mwesigwa
Diwani wa kata ya Bukomela Kulwa Shoto
Jumla ya Vijana 15 kutoka halmashauri ya ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamepatiwa mtaji wa shilingi milioni moja na nusu, ili kuanzisha shughuli za ujasiriamali, na kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuwasababishia maambukizi ya UKIMWI.

Fedha hizo zimetolewa juzi mjini Kahama na shirika la HUHESO FOUNDATION kwa ufadhili wa kamati ya kudhibiti UKIMWI ya halmashauri ya Ushetu, ambapo vijana hao kutoka kata 15, kila mmoja amepewa shilingi laki moja taslimu.

Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, diwani wa kata ya Bukomela Kulwa Shoto amesema halmashauri hiyo imetoa fedha hizo ili kusaidia vijana kujishughulisha na kujikinga na vishawishi vinavyoweza kuwasababishia maambukizi ya UKIMWI.


Shoto ambaye alimuwakilisha mwenyekiti wa kamati ya kudhibiti ukimwi ya halmashauri hiyo Tabu Katoto, amewataka vijana hao kuzitumia fedha hizo kama walivyoelekezwa, ili kuiwezesha halmashauri kuendelea na utaratibu huo wa kusaidia vijana. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa HUHESO FOUNDATION Juma Mwesigwa ameahidi kuwa shirika lake litaendelea kufuatilia fedha hizo zimetumikaje, huku akiitaka halmashauri hiyo kuweka mpango wa kuwaongezea mitaji watakaotumia fedha hizo vizuri.



Fedha hizo zimetolewa kwa vijana 10 kutoka katika kata 10 pekee,ambao wamelishukuru shirika hilo kwa msaada huo, huku wengine watano kutoka katika kata 5 wakiwa hawakuhudhuria katika shughuli hiyo.


Na Faraji Mfinanga-Kahama 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com