Vijana wawili wameuawa kwa kushambuliwa na wananchi wenye hasira mkoani Geita kwa kile kilichotajwa kuwa vijana hao walimuua mama yao wa kambo kwa kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Akizungumzia tukio hilo kaimu Afisa mtendaji wa kata ya Busanda alisema tukio hilo lilitokea jana katika kijiji cha Nyamtundu majira ya saa tatu usiku ambapo Mama moja aliyejulikana kwa jina la Mwanamaila Mwanatenga (50) aliuawa kwa kukatwa katwa mapanga na watu wasiojulikana wakati akitoka chooni kujisaidia mara baada ya kumaliza kula.
Alisema mara baada ya kufanya mauaji hayo walitokomea kusikojulikana na wananchi kwa kushirikiana na jeshi la Sungusungu walianza msako wa kuwatafuta na hatimaye waliwakamata wakijaribu kutoroka.
Watuhumiwa hao walikamatwa katika kijiji jirani cha Msasa wakiwa na damu kwenye makoti waliyokuwa wamevaa ndipo wananchi hao wakiwa na jeshi la sungusungu waliwauliza kuwa wanatoka wapi.
Watuhumiwa hao walijibu kuwa wanatoka kwenye sherehe ya harusi kwao na baada ya wanafamilia kubaini kuwa mama yao wa kambo ameuawa walianza kuwapiga hadi kuwaua na kisha wakawababua kwa moto.
Afisa huyo aliwataja waliokufa kuwa ni Makoye Nzari(25) na Masumbuko Nzari(36) wote wakiwa ni watoto wa kambo wa mama huyo.
Diwani wa kata hiyo Aliphonce Matonange amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kamanda wa jeshi la polis mkoani Geita Joseph Konyo alisema hakuna aliyekamatwa juu ya tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea wa kuwabaini waliofanya tukio hilo na huku akiwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Na Valence Robert- Malunde1 blog-Geita
Social Plugin