Mkuu wa mkoa wa Geita Saidi Magalula akizungumza na wachimbaji wadogo wa Geita-Picha na Valence Robert-Malunde1 blog Geita |
Zaidi ya Wachimbaji wadogo 2000 wa kijiji cha Samina Mkoani Geita wamefunga barabara kuu ya gari za kuelekea Mwanza Bukoba, kwa muda wa saa 5 baada ya kuzuiliwa kufanya shughuli za Uchimbaji Katika Mlima wa Samina wakishinikiza uogozi wa serikali ya Mkoa kwenda kuwasikiliza.
Tukio hilo limetokea jana ambapo wachimbaji hao walikaa barabarani takribani masaa matano huku wakizuhia gari za migodini kukatiza eneo la barabara hiyo jambo lililosababisha magari ya migodini kushindwa kupita barabara hiyo na kurudi zilikotoka.
"Sisi tumeamua kukaa barabarani tumsubiri Mkuu wa mkoa wa Geita Saidi Magalula, tumeambiwa anakuja kutusikiliza na sisi hatutoki hapa mpaka tumuone anakuja maana amekuwa akitoa ahadi kila siku anakuja lakini hatumuoni”alisema Masenya Elias Mchimbaji mdogo.
Walisema kuwa wachimbaji hao walizuiliwa kufanya kazi katika mlima ambao unamilikiwa na kampuni ya Uchimbaji wa Dhahabu ya Geita(GGM) tangu tarehe 4 mwezi Julai mwaka huu na kampuni hiyo ambapo wachimbaji hao walipewa siku 3 kuondoka jambo walilolilalamikia kuwa ni ghafla sana.
" Kwanza hatukupewa taarifa mapema na serikali ,kwamba tunatakiwa kuondoka ,tulistukia tu GGM inakuja na kutupa siku Tatu.Juzi tarehe 9 mwezi julai mwaka huu walikuja askari na kutufukuza kwa kurusha mabomuambayo yalikuja na kuanguka kwenye makazi ya watu"alisema Kulwa Joseph .
Walisema kuwa siku ambayo walirusha mabomu mmoja ilianguka kwenye nyumba ya mkazi wa eneo hilo Pili Yohana hali iliyosababisha eneo la nyumba yake kushika moto.
"ilikuwa saa 9 mchana nikasikia kitu kama mlipuko nikajua kuwa wanalipua mgodini ghafla nikaona kitu kinakuja hewani kinatoa moshi kikaanguka hapo kwenye nyumba na mimi nilikuwa pembeni naosha mtoto nikakimbia"alisema mtoto wa mama huyo Julius Yohana (8)
Alisema kitu kitu hicho kilipiga nguzo ya nyumba ambayo ilikuwa bado inaezekwa kisha kuanguka chini ambapo moto uliwaka na watu wakaja kuuzima kwa majani ya miti na maji.
Hata hivyo baada ya kukaa muda wote barabarani baadae Mkuu wa mkoa aliwasili eneo hilo la barabara majira ya saa 6:00 mchana na kuwataka waondoke eneo hilo ili wakazungumze.
Wachimbaji hao walikubali na kwenda eneo la senta ya kijiji hicho ,ambapo Mkuu wa Mkoa alizungumza nao na kuwaeleza kuwa wampe siku tano kisha atawapa jibu ni wapi wataenda kufanya shughuli zao za uchimbaji.
"Naomba mnipe siku tano nitawapa jibu,lakini ndani ya siku tano hizi sitaki niwaone mnaenda mlimani kuchimba kwani eneo hilo siyo la kwenu ni mali ya GGM na kama mnavyojua GGM wapo kisheria katika eneo hilo"alisema Magalula.
Hata hivyo kauli hiyo hawakukubaliana nayo kwani wao walitaka waendelee kuchimba wakati serikali ikiwatafutia eneo na kusema kitendo alichofanya Mkuu wa Mkoa siyo cha kiungwana .
"Sasa tunasema hivi mkuu wa mkoa aandae makaburi ya kuzika watu wa samina,sisi tunategemea huo mlima kupata riziki yetu ,hizo siku tano tutakula wapi"walisikika wakisema wachimbaji hao.
Na Valence Robert-Geita
Social Plugin