Watu wawili wamekamtwa kwa tuhuma za mauaji ya Sista Clesencia Kapuli (50) wa Kanisa Katoliki, aliyekuwa Mhasibu katika Shule ya Sekondari Mwenyeheri, jijini Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema watu hao ni kati ya watu wanane waliokamatwa kwa tuhuma za ujambazi sugu wa kutumia silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema watu hao walikamtwa juzi katika operesheni iliyofanywa na jeshi hilo kwa kutumia vikosi maalum.
Alisema licha ya majambazi hao wawili kuhusika katika tukio la mauaji ya sista huyo, lakini pia walihusika katika tukio la kupora fedha katika benki ya Barclays tawi la Kinondoni miezi michache iliyopita.
Aliwataja waliohusika hao wa mauaji ya Mtawa kuwa ni Manase Ogenyeka (35), mkazi wa Tabata na Hamis Ismail, mfanyabisahara na mkazi wa Magomeni Mwembechai.
Watuhumiwa wengine ni Beda Mallya (37), mkazi wa Mbezi Msakuzi; Michael Mushi (50), mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makabe; Sadick Mohamed (32), mfanyabiashara, mkazi wa Mbagala Kizuani; Elibariki Makumba (30); Nurdin Suleiman (40), wote wakazi wa Buguruni Madenge, pamoja na Mrumis Saleh (38), mkazi wa Kigogo Freshi.
Pia Jeshi la Polisi limesema linaendelea na operesheni hiyo pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio la maujai ya sista Kapuli, Juni 23, mwaka huu, pamoja na jambazi mmoja aliyehusika katika tukio la wizi wa fedha katika benki ya Barclays.
Sista huyo ambaye alikuwa mhasibu wa Shule ya Sekondari Mwenyeheri iliyopo Makoka wilayani Kinondoni, aliuawa Juni 23, mwaka huu kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazio waliokuwa katika pikipiki aina ya Boxer.
Sista Kapuli alivamiwa na majambazi hao baada ya kutoka benki Mlimani City akiwa katika gari aina ya Pick up double cabin yenye namba za usajili T 213 CTZ.
via>>Nipashe
Social Plugin