KAIMU Afisa Habari wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza Thomas Lutego amewafukuza Waandishi wa Habari wa Gazeti la Tanzania Daima Antony Sollo na Valence Robert pamoja na Twallad Sallum wa Gazeti la Mwananchi waliofika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Misungwi ambako kikao cha Baraza la Madiwani kilikuwa kikifanyika hapo.
Waandishi hao waliwasili katika ukumbi huo na kukuta kikao cha Baraza la Madiwani kikiendelea na kuingia kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kupasha habari kwa jamii, ghafla Lutego aliwaita waandishi hao na kuwaeleza kuwa hawaruhusiwi kushiriki kikao hicho kwa kuwa alikuwa amealika waandishi wa habari vyombo vingine.
“Naomba mtoke ninyi mmealikwa na nani?mimi nilikuwa nimealika waandishi wane tu sasa nawaonya iwapo mtaendelea kukaa na kufanya shughuli zenu hapa mtaona nitakachowafanya.”alisema Lutego.
Baada ya kutokea kwa mtafaruku huo Waandishi walitoa ripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mariam Lugayila ili aweze kuwapa mwongozo,Lugayila alisema.....
“kikao hiki ni kikao cha wazi sasa kwa nini awazuie? Jamani mimi msije mkaninukuu ila ninavyofahamu mimi kikao hiki ruksa mtu yeyote kuhudhuria na kufuatilia mambo mbalimbali.”inakuwaje sasa mtu achukue jukumu la kufukuza wanahabari?
Hali hii si mara ya kwanza kwa Afisa Habari huyu kufanya fitna kwa waandishi wa Habari na inaonekana kuna kitu kinachofichwa na Afisa Habari huyo ili watu wasijue kinachoendelea katika Halmashauri hiyo.
Imedaiwa kuwa halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imekuwa na matukio mengi ya ufujaji wa fedha za umma na huenda kualika waandishi kwa ubaguzi ni moja ya njia ya kuzuia na kuficha maovu hayo na wameomba Mkurugenzi wa Halmashauri achukue hatua kutatua mgogoro huo kama na yeye hahusiki kwa namna moja au nyingine katika suala la kuzuia waandishi.
Naye Diwani wa Kata ya Usagara Costantine Kilaga alisema “huyu bwana atakuwa na maslahi binafsi juu ya jambo hili hiki ni kikao huru na ni cha wazi sasa kwa nini azuie waandishi?alihoji Kilaga”
Katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichopita Lutego alitoa taarifa za kutumia kiasi cha shilingi laki sita 600,000 tu kati ya shilingi milioni nane 8,000,000. zinazotengwa na Halmashauri ya kwa ajili ya masuala ya Habari kwa mwaka 2013.
Hali hii inaonyesha jinsi anavyowanyima haki ya kupata habari wananchi wa Wilaya ya Misungwi na pia ni ushahidi tosha kwamba kuna siri kubwa inayofichwa na huenda siyo maamuzi yake ila kuna kitu nyuma yake.
Wakiendelea kutafuta haki yao ya kuhudhuria kikao hicho,waandishi wa Habari hao walimpa taarifa Mbunge wa Jimbo la Misungwi Charles Kitwanga juu ya kunyimwa haki hiyo ambapo Kitwanga alimwita Afisa habari huyo na kumhoji na baada ya muda Lutego alionekana kulegeza msimamo wake huo na kuwaacha waandishi hao kuendelea na majukumu yao.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Nathan Mshana alipoulizwa iwapo kuna uhalali juu ya kauli iliyotolewa na Kaimu Afisa Habari Thomas Lutego kuzuia waandishi kuingia katika kikao cha Madiwani hao Mshana alisema hana cha kuzungumza juu ya jambo hili alijibu kwa mkato “Kikao hiki ni cha wazi na kwamba kila mtu anayo haki ya kuingia katika kikao hicho.”alisema Mshana.
Chanzo cha taarifa hizi kinaendelea kufuatilia kujua undani wa chanzo cha ubaguzi kwa wanahabari unaofanywa na Afisa Habari huyo kwa kuita waandishi kirafiki huku akiacha kuwaalika wanahabari wengine kuhudhuria vikao mbalimbali vya Halmashauri hiyo.
Na Waandishi wa Malunde1 blog-Misungwi
Social Plugin