Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt,Ntuli Kapologwe amewatoa hofu wananchi wa mkoa wa Shinyanga juu ya uvumi wa kuingia kwa ugonjwa hatari wa Ebola mkoani Shinyanga.
Mganga huyo wa mkoa amewatoa hofu wananchi kufuatia kuenea uvumi kuwa kuna mgonjwa wa Ebola aliyefikishwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kutoka moja ya mitaa katika Manispaa ya Shinyanga.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu huyo mgonjwa huyo ambaye alikuwa akitokwa damu mdomoni na puani alifika hospitalini hapo Agosti 12 mwaka huu na mara baada ya kufika wauguzi na madakitari walitaharuki.
Mgonjwa alilazimika kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) huku baadhi ya wauguzi na madaktari wakimkimbia hali iliyotia hofu kwa baadhi ya wahudumu na hata wagonjwa hospitalini hapo.
Hata hivyo Mganga Mkuu huyo alisema hakuna mgonjwa wa Ebola na kuwataka wananchi waamini hivyo na kuwa uongozi wa mkoa umejipanga kukabiliana na ugonjwa.
Alisema mgonjwa aliyepokelewa ana matatizo ya kutokwa damu mara kwa mara na kuwa baada ya uchunguzi wa awali imebainika siyo Ebola.
Hata hivyo katika kukabaliana na ugonjwa huyo waganga wakuu katika halmashauri zote 6 za wilaya za mkoa wamekubaliana pindi atakapogundulika mtu mwenye dalili za ugonjwa huo taarifa itolewe mara moja katika ngazi ya mkoa na kuna timu maalum ya kushughulika na ugonjwa huo hatari.
Alisema mara baada ya taarifa kutolewa timu hiyo ndiyo itakayo thibitisha kama kweli mgojwa huyo ana dalili zote za ebola na taarifa kutolewa.
Mganga huyo pia alisema hospitali zote katika halmashauri za mkoa wa Shinyanga zimepewa maelekezo juu ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin