Madiwani walioasi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamerejea na kudai walirubuniwa na makada watano wa CCM kuhama kwenye chama hicho ili wawatumie kuwaua, Dk. Willbrod Slaa na John Mnyika.
Madiwani hao ni Sebastian Mzuka wa kata ya Ngokolo na Zacharia Martin Mfuko wa kata ya Masekelo wote kutoka Shinganya mjini ambao wamewataja makada hao kuwa ni Naibu wa Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Wengine ni Naibu waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga mjini, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC, chama tawala, Nape Nnauye, na Habibu Mchange (aliyefukuzwa Chadema).
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika ofisi za chama hicho, madiwani hao walisema kuwa, mauaji hayo yalipangwa kutekelezwa kwa kiasi cha Sh. milioni 180.
Diwani Mzuka alisema wamefika kwenye ofisi hizo ili kueleza kinachoendelea kudhoofisha chama na kuomba toba baada ya kuhama.
Alisema mara baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuvuliwa madaraka Chadema, Mchange alipewa kazi (dili) na CCM kutafuta viongozi na madiwani wa Chadema lengo likiwa ni kukidhoofisha.
Alisema Mchange aliwafuata Shinyanga kuzungumza nao kuhusu suala hilo.
Alisema Januari 27, mwaka huu alipewa kazi ya kulipua helkopta iliyokuwa ikitumiwa na Katibu Mkuu Chadema, Dk. Slaa, Mbunge wa Ubungo, Mnyika na Mwenyekiti wa kanda ya Mashariki katika ziara ya Kanda ya Ziwa.
“Aliniambia kuwa Masele ana dili la shilingi milioni 180, baada ya ujumbe huo nilipokea simu ya waziri huyo ambaye aliniambia nikifanikisha nitalipwa fedha hizo,” alisema.
Alisema kuwa Masele alimtaka aeleze helikopta hiyo itatua wapi, muda gani na kama kweli wahusika wamo ndani yake kisha ulipuaji ufanywe na watu walioandaliwa.
Alisema alijiandaa na kufuatilia ila hofu ya kimungu ilimuingia akahofia taifa litapokeaje tukio la kifo cha Dk. Slaa na yeye akihusika.
“Nilimweleza Masele lakini alimpigia simu mkuu wa wilaya ya Shinyanga Anna Rose Nyamubi, ambaye alimshauri kuwa sio vyema tukio hilo likafanyika wilayani kwake, baadaye nilikutanishwa na katibu mkuu wa umoja wa vijana ccm (UVCCM) Taifa , Sixtus Mapunda pamoja na mtu mmoja wa usalama, ” alisema.
Aidha, alisema aliwashauri badala ya kulipua watumie mabango na kurubuni vijana kuhujumu ziara ya Dk. Slaa ambapo walifanikisha hilo.
Alisema baadaye walikutana tena na Nape, Nchemba na kuombwa wawashawishi madiwani na viongozi wengine wahamie CCM kwa ahadi ya kupewa ukatibu wa Wilaya kwenye wilaya watakazoamua.
Alisema baadaye madiwani hao walienda Mwanza mjini ambapo huko walikutana na Nape ambaye alieleza kusikitishwa kitendo cha Chadema kumvua uwanachama Zitto.
KUONDOKA CHADEMA
Alisema Februari 26, mwaka huu waliondoka rasmi Chadema ambapo Nape alifika huko na kukutana naye hoteli ya Kalena ambapo katika mazungumzo alimhakikishia maisha mazuri pamoja na uongozi.
“Usiku ulipofika gari la mwenyekiti wa mkoa wa Mwanza iliwachukua na kuwapeleka uwanja wa ndege na kusafiri kuja Dar es Salaam kukutana na Nchemba ambaye naye aliwataka waelekee Dodoma na baadaye Kalenga,” alisema.
Aliongeza kuwa Dodoma walienda nyumbani kwa Kinana ambaye huko waliwakuta Masele, Nchemba na Mchange ambapo wakati wote Katibu Mkuu alisifu kitendo chao cha kuondoka Chadema.
Alisema katika mazungumzo makada hao walimwambia Nchange asichoke kwa kazi anayofanya.
ACT YATAJWA
Mzuka alisema makada hao walikubaliana mgogoro ndani ya Chadema lazima uboreshwe na kuahidi kugharamia fedha za kwenda mikoani na pia wakasema kuna chama kitasajiliwa.
Pia alisema makada hao walisema watahakikisha Msajili wa vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi anakipatia usajili wa kudumu kwa gharama yoyote chama cha ACT ili CCM ipate ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Alisema katika mazungumzo hayo, Kinana alisema ACT imeanzishwa kwa lengo maalum la kuipa CCM ushindi kwa kuwa hata huko duniani, ushindi wa chama tawala unatokana na usajili wa vyama vipya.
WABUNGE WANNE KUHUJUMIWA
Makada hao walikubaliana katika uchaguzi ujao mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, asirudi bungeni kwa sababu ameitia hasara serikali kuhusu hoja zake dhidi ya katiba.
“Katika jimbo la Lissu, ACT itafadhiliwa kusaidia kutoa mgombea CCM ambapo itagawa kura za jimbo,” alisema.
Diwani huyo alitaja wabunge wengine ambao wapo kwenye mtego huo kuwa ni mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema ambaye imeelezwa amesababisha kushuka kwa utalii.
Wengine ni mbunge wa Iringa mjini Mchugaji Peter Msigwa na mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi.
Kwa upande wa Lissu alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Diwani akijiuzulu anatakiwa aandike barua rasmi kwa mwenyekiti wa Halmashauri na kuambatanisha na kiapo.
“Hawa hawakufanya hivyo kwa hiyo bado ni madiwani wa halmashauri ya mji wa Shinyanga,na uthibitisho kuwa hawajajiuzulu ni kuwa siku 90 zimepita bila kutangazwa uchaguzi, “ alisema.
via nipashe
Social Plugin