LORI LILILOBEBA PAMBA LAPINDUKA SHINYANGA,MMOJA AFARIKI DUNIA,MAJERUHI WANNE,WALIKUWA WAMEPANDA JUU YA GARI HILO

NB-picha haiendani na habari hapa chini,lakini ni mfano magari yanayobeba pamba na watu kupanda juu-Picha kutoka maktaba ya Malunde1 blog
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Rashid Juma(25) amefariki dunia papo hapo baada ya gari alilokuwa amepanda juu na wenzake likiwa limebeba pamba kuacha njia na kupinduka katika barabara ya Shinyanga kuelekea Pandagichiza  katika kijiji cha Shilabela kata ya Pandagichiza,tarafa ya Mondo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga

Lori hilo lenye namba za usajili T214 AGV aina ya scania lori mali ya kampuni ya Afrisian Ginnery ya Shinyanga likitoka Nindo kwenda Shinyanga mjini  likiendeshwa na  Justine Philemon(35) mkazi wa Majengo mjini Shinyanga,aliyetoroka baada ya ajali  liliacha njia na kupinduka jana saa 2:40 asubuhi.

Kamanda  wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha amesema baada ya lori hilo kupinduka Rashid Juma aliyekuwa amepanda juu ya gari alifariki dunia papo hapo huku wenzake wanne wakijeruhiwa katika sehemu mbalimbali za miili yao na wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga.

Amewataja majeruhi hao kuwa ni Daniel James(18) Philipo Charles(19)na Richard Samwel (19) wote wakazi wa Ibadakuli na Charles Peter(19) mkazi wa Kolandoto.


Amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi huku akitoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazozuilika.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post