Watu wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi Mkoani Iringa kwa tuhuma mbalimbali ikiwepo ya mtu mmoja kushikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma ya kumnywesha pombe mtoto wa miaka 14 kisha kumbaka.
Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani Iringa ACP Ramadhani Mungi amemtaja mtuhumiwa kuwa ni Sepelwa Mnyambala umri miaka 25 mkazi wa eneo la kihesa Sokoni Manispaa ya Iringa anashikiliwa kwa tuhuma ya kumnywesha mtoto huyo pombe aina ya kiloba kisha kumfanyia unyama huo.
Ameongeza kuwa mtoto huyo ni mkazi wa eneo la Kihesa Manispaa ya Iringa.
Hali hiyo iliyosababishia maumivu makali mtoto huyo huku chanzo cha tukio hilo kikiwa ni tamaa ya mapenzi.
Katika tukio la pili Kamanda Mungi amesema Mohamed Mfilinge umri miaka 20 mkazi wa Kijiji cha Dinginayo wilaya ya Kilolo Mkoa wa Iringa amekamatwa akiwa na pikipiki aina ya Shineray mali ya wizi akiwa katika harakati za kuiuza chanzo kikiwa ni tamaa ya mali.
Aidha amesema jeshi la polisi linawatafuta mtu/watu wasiofamika kwa tuhuma ya kuiba pikipiki yenye namba za usajili T.645 CNP aina ya Sunlg yenye thamani ya shilingi 1,700,000 mali ya Modestus Ngusi umri miaka 31 mkazi wa eneo la Makorongoni Manispaa ya Iringa.
Hata hivyo Kamanda Mungi amesema katika maeneo ya Mivinjeni Manispaa ya Iringa nyumba ya Merina Msigala umri miaka 25 imeungua moto baada ya mtoto wa mpangaji kuchezea kiberiti na kuwasha godoro na ikapelekea nyaya za umeme kushika moto huo ambapo hasara yake ni shilingi milioni nne.