Siasa noma_ MGOMBEA WA CHADEMA GEITA ACHEZEWA MCHEZO MCHAFU




Kambi ya katibu wa Jimbo la Geita  kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)Rogers Luhega imegeuka kuwa ya vituko katika uchaguzi unaoendelea wa ngazi ya jimbo baada ya majina ya wagombea wasiomuunga mkono kuondolewa kwenye kinyang'anyiro bila sababu za msingi na pasipo kutaja sababu ya kufanya hivyo.


Katika usaili wa jana ulikokuwa unaendelea wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chadema jimbo la Geita kwenye Hoteli ya Brightday,uligubikwa na mizengwe  ya hapa na pale.

Mapema asubuhi tetesi za majina ya wagombea wanaokubalika kwa wajumbe wengi wa chadema ambao wanapinga mienendo ya Luhega ya kukigeuza chama kama mali yake binafsi kukatwa ziligubika anga la mji wa Geita huku shauku ya wengi ikisubiri majina yabandikwe ili wahoji sababu za kuwaengua.

Majira ya saaa 4:45 usiku kazi ya kusaili majina ya wagombea ilikamilika na katibu wa chadema kanda ya ziwa magharibi Robart Bujiku alianza kutangaza majina ya wagombea waliopita katika usaili huo.

Katibu huyo aliyekuwa anasaidiana na mwenyekiti wa muda wa chadema mkoa wa Geita Alphonce Mawazo,kabla ya kuita majina alichimba mkwara kwa wanachama hao kuwataka wakubali matokeo kwa wale watakaokuwa wamechujwa katika usaili huo.

Hata hivyo baadaye katibu Bujiku aliwatoa wasiwasi wanachama hao kuwa,majina yao yamepita na nafasi walizoomba na kwamba iwapo kuna makundi yasiendelee tena kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuwa chadema.

Hata hivyo pamoja na kudai hivyo,baada ya kusoma majina hayo baadhi ya wagombea walijikuta wakiondolewa kwenye nafasi walizoomba katika jimbo bila sababu za msingi.

Mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa jimbo Jackson Jonathan Mabula ambaye ndiyo tarajio la wajumbe wengi kwa msimamao wake wa kutopenda rushwa na kusimamia ukweli aliondolewa kwenye nafasi hiyo.


Chanzo chetu cha habari kimebaini kuwa,sababu za Jonathan kuondolewa katika kinyang'anyiro hicho ni kuwatengenezea mazingira haramu ya ushindi wagombea dhaifu akiwemo Diwani wa kata ya kalangalala Peter Donald ambaye wanachama hawana imani nao.

Mbali na Donald aliyeomba nafasi ya uenyekiti wa jimbo,mwingine ni Albart Machumu aliyeomba nafasi mbili ya jimbo na wilaya na zote aliteuliwa tofauti na Jonathan ambaye mbali na kuomba nafasi mbili moja alienguliwa na hata alipolalamika alijibiwa kejeli.

''Wewe uongozi umeshaamua hivyo,kukuondoa kwenye nafasi hiyo hivyo hakuna jinsi na kama hujaridhika unaweza kukata rufaa''alisikika Bujiku akimweleza Jonathan mbele ya mwandishi wa habari hizi aliyekuwa anafuatilia mchujo huo.

Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi chadema waliokuwa eneo hilo walisikika wakilaaani hatua ya kuondolewa kwa Jonathan na kutishia kuupinga uchaguzi huo mahakamani iwapo hawatamtendea haki mwenzao kwa walichodai wamechoshwa kuwa wasindikizaji.

''Tumechoka kuwa wasindikizaji.......wagombea wazuri mnawaengua mnabakiza wale hawauziki, je hii ni halali na kwa staili hii tutaiondoa ccm madarakani!!...hatukubali msipotenda haki kwa mwanachama mwenzetu tutaupinga mahakamani uchaguzi wa jimbo''walisikika baadhi ya wanachama wakilalama

Kwa sasa Luhega anaonekana kuchanganyikiwa baada ya kuona nafasi yake inazidi kutitia ambapo hivi karibuni baada ya matokeo ya awali kuvuja na  kuonyesha kuwa   waliokuwa wameshinda kwenye uchaguzi wa kata ya  Kalangalala alioufuta,wajumbe wengi wanaomuunga mkono mgombea ukatibu wa Jimbo Mutta Robert na kuonyesha kuwa Ruhega anapoteza nafasi nyingi katika uchaguzi huo.

Uchaguzi huo wa kata uliitishwa kama uchaguzi wa marudio baada ya katibu huyo wa Jimbo kutangaza kuwa uchaguzi wa kata hiyo kufutwa kwa madai kwamba uchaguzi haukufuata katiba ili hali si kweli.

Wakati madai hayo yanaibuka ya kutofuata katiba,kuna barua zilizotoka kwenye matawi mbalimbali zikionyesha kuwa barua za kulalamikia uchaguzi huo ziliandikwa na wafuasi wa katibu huyo kwa ushawishi wake ili autengue na kuitisha upya ili ajipange vizuri baada ya kubaini waliokuwa wamechaguliwa walikuwa hawamuungi mkono katika uchaguzi wa Jimbo.

Inadaiwa kuwa katika mkakati huo wa kufuta baadhi ya wagombea na kufuta uchaguzi ili kuhakikisha wanapenyesha watu wake,unaratibiwa kwa msaada wa kiongozi wa Kanda Robert Bujiku anayedaiwa kuandaa njama za kumrudisha madarakani katibu huyo kwa hila.

Hata hivyo,jana baada ya katibu huyo wa Jimbo kutangaza kufuta uchaguzi huo bila sababu, wanachama wengi wa kata hiyo na kata za jirani waliokuwa wakifuatilia uchaguzi huo walijaa jazba na kuanzisha zogo kubwa na kusababisha baadhi ya wafuasi wa chadema kuanza kurusha maneno makali na kutishia kuchoma moto gari lake.

Wakati hayo yakiendelea,Katibu huyo,na wapambe wake akiwemo Neema Chozaile,Nguru Brighton walikuwa wamejifungia kwenye moja ya vyumba vya ofisi za jengo hilo lililokuwa likifanyikia uchaguzi huo wakihofia kupigwa na wanachama ambao walikuwa na jazba wakipinga katibu huyo kutumia mamlaka yake kufuta uchaguzi huo.

Wafuasi hao walitulizwa na mgombea mwenzake Mutta Robert aliyeonekana kusikilizwa na wafuasi wengi wa chadema.


Katibu huyo na viongozi wenzake walilazimika kujifungia ukumbini huo na kuita askari polisi na kuondoka hapo chini ya ulinzi mkali wa askari hao.

Hivi karibuni Luhega amekaririwa akisema kuwa ameisha fanya mazungumzo na Chagulani mfuasi wa chama cha ACT anayeshi Mwanza kwa madai kwamba ameombwa kuhamia chama hicho.

Wanachama wengi wa chadema mjini Geita wamepoteza imani na Katibu huyo baada ya kupata tetesi kuwa ni shemeji yake na Zitto Kabwe na anajiandaa kuhamia ACT.

“Katibu amekuwa na matatizo mengi na amekuwa akikwamisha shughuli za chama na kupanga mikakati michafu ya kuleta migogoro ndani ya chama bila sababu za msingi na chama amekigawa katika makundi makundi,na suluhisho la haya yote ni kumuondoa katika nafasi hiyo na bila kumuondoa chadema haipo Geita” alisema kiongozi mmoja wa kamati tendaji ya Jimbo la Geita.

Alhamis ya wiki iliyopita vijana wa ulinzi wa chadema (Red Brigade) wakiwa na waandishi wa habari walikuta wafuasi wa katibu huyo katika Hoteli ya Wandela mjini Geita wakiwa wmekusanyika kama 50 wakinywa soda na vyakula mbalimbali na kukiri kwamba wameitwa kuweka mikakati ya ushindi.


Ruhega inadaiwa anajitengenezea njia ya ushindi kwa kuwashawishi wajumbe kwa pesa,vinywaji na chakula na kumtumia katibu wa Kanda Robert Bujiku, ambaye ni rafiki yake kutuma taarifa za uongo makao makuu ya chadema kuwa wagombea wenzake na mamluki kutoka chama cha mapinduzi (ccm).

Na Victor Bariety-Malunde1 blog-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post