TAARIFA KAMILI KUHUSU BINTI ALIYEANGUKIWA JIWE KUBWA NA KUFARIKI DUNIA HUKO KAHAMA AKICHIMBA KOKOTO

Wananchi wakiangalia jiwe lililomwangukia na kumfunika Marehemu Lucia Bahati
Afisa mtendaji wa Kijiji cha Shunu Benjamin Makelo akielezea tukio hilo lilivyokuwa.
Mkazi wa kijiji cha Shunu kata ya Nyahanga Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, Lucia Bahati (25) amefariki dunia papo hapo baada ya kuangukiwa na jiwe katika eneo lililokuwa likitumika kutengeneza kokoto kijijini humo. 


Tukio hilo limetokea jana majira ya saa nne asubuhi wakati Lucia na wenzake wakichimba kokoto katika eneo hilo lililopo katika kitongoji cha Ikorongo ambalo liliwekwa mashine za kutengeneza kokoto wakati wa ujenzi wa Barabara za lami wilayani Kahama. 

Kwa mujibu wa Angela Alex ambaye walikuwa wakichimba kokoto katika eneo hilo na Marehemu, jiwe hilo lilikuwa limekaa vibaya na kwamba walikuwa wakifanya kazi kwa tahadhari kabla ya kumuangukia mwenzake. 

Afisa mtendaji wa Kijiji cha Shunu Benjamin Makelo, amesema baada ya tukio hilo, wananchi walifika kusaidia kusogeza jiwe hilo na kuutoa mwili wa Lucia ambaye ni mzaliwa wa Ilogi wilayani humo, akiwa tayari ameshafariki. 

Makelo amesema awali baada ya kupata taarifa za tukio hilo alipiga simu polisi ambao baadae walifika na kuuchukua mwili wa marehemu ambao sasa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya ya Kahama. 


Kufuatia tukio hilo, Afisa mtendaji wa kata ya Nyahanga William Upamba amesitisha shughuli za uchimbaji wa kokoto katika eneo hilo ambalo ni hatari kwa maisha ya watu, na ametoa siku 10 kwa wenye kokoto zao kuhakikisha wameziondoa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post