Picha kutoka mktaba ya Malunde1 blog-Huyu ni mzee jina tunalo akionesha majeraha baada ya kucharangwa mapanga na vibaka katika daraja la Mhumbu barabara ya Shinyanga-Mwanza
Wakazi wa Shinyanga mjini wameingiwa na hofu kubwa kutokana wimbi la vibaka kuzagaa katika maeneo mbalimbali wakiwa na mapanga,fimbo na virungu nyakati za usiku na kukaba,kujeruhi kisha kupora mali za wananchi.
Walisema tofauti na eneo la daraja la Mhumbu lililoko kata ya Ibadakuli na kule Ndala katika manispaa ya Shinyanga hivi sasa vibaka wamehamia katika daraja la Buluba,barabara karibu na Shule ya Sekondari Buluba,eneo la shule za msingi Bugoyi A na B lakini pia eneo linalozunguka kanisa katoliki la Ngokolo katika manispaa ya Shinyanga.
“Inatupa mashaka sana,tunanyang’anywa simu,pesa na vitu mbalimbali,tunacharangwa mapanga,tunaomba vyombo vya ulinzi na usalama vitusaidie,haiwezekani kuanzia saa mbili watu vibaka wajitawale namna hii”,waliongeza wananchi hao.
Mmoja wa wananchi hao (jina tunalo)alisema juzi alishuhudia mwanamke akipiga kelele za kuomba msaada majira ya saa mbili usiku katika maeneo ya shule ya sekondari Buluba ambapo mwanamke huyo alikuwa amekabwa na vibaka huku wakiwa na mapanga.
Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga kamishina mwandamizi wa polisi Justus Kamugisha alisema jeshi lake limejipanga vyema kudhibiti vibaka hao na kuwatia nguvuni na kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwani wanahatarisha amani ya wakazi wa manispaa ya Shinyanga.
Alisema katika kufanikisha harakati hizo aliwataka wananchi washirikiane na jeshi hilo kwa kutoa taarifa dhidi ya wahalifu pamoja na maeneo wanayopendelea kujificha.
“Ndugu zangu jeshi la polisi haliwezi kufanya kazi peke yake pasipo kushirikiana na wananchi ambao ndio hufanyiwa vitendo hivyo vya kukabwa na vibaka na kuporwa mali zao,tunawaomba wananchi kushirikiana nasi,ili kukomesha wahalifu”,alisisitiza kamanda Kamugisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na malunde1 blog baadhi ya wanachi walisema vitendo vya ukabaji vimekuwa vikifanywa na baadhi ya vijana kuanzia nyakati za saa mbili mjini Shinyanga. |
Ndani ya wiki moja katika manispaa ya Shinyanga kumeripotiwa matukio sita ya uhalifu ambayo hufanywa na vibaka, kwa kukaba watu na kuwanyang’anya mali zao na wanaokuwa wagumu kutoa mali basi huambulia kuwajeruhiwa kwa kuwakata na mapanga katika sehemu mbalimbali za miili yao na kisha kuwapora kwa nguvu.
Na Kadama Malunde-Shinyanga