Twaweza waibua mambo_RUSHWA NI JAMBO LA KAWAIDA KATIKA SEKTA ZOTE ZA HUDUMA ZA SERIKALI,POLISI WANAONGOZA KWA RUSHWA


Twaweza.org

Taarifa kwa Vyombo vya Habari | Press Release: Sauti za Wananchi


5 Agosti 2014, Dar es Salaam: Wananchi wanaiona rushwa katika sekta zote za huduma za Serikali kama kitu cha kawaida kabisa. Sekta zinazoongoza kwa rushwa ni pamoja na polisi (94%), siasa (91%), afya (82%), kodi (80%) , ardhi (79%), elimu (70%), serikali za mitaa (68%) na maji (56%).

 Pia wananchi 50% wanaona mashirika yasiyo ya kiserikali nayo yanajihusisha na rushwa. Sekta pekee zinazoonekana kuwa na viwango vya rushwa chini ya 50% ni zile za biashara pamoja na mashirika ya dini.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wenye jina la Je, juhudi za serikali zimesaidia vita dhidi ya rushwa? Mtazamo wa watu kuhusu rushwa nchini Tanzania

Muhtasari umetokana na utafiti wa Sauti za Wananchi; utafiti wa kwanza Afrika kwa njia ya simu mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa, ambao ulikusanya maoni kutoka Tanzania Bara.

Mbali na mitazamo kuhusu rushwa, Twaweza iliuliza kuwa ni wakati gani hasa wananchi huombwa rushwa? Kwa mara nyingine, polisi waliongoza katika hili: wananchi watatu kati ya watano (60%) waliombwa rushwa mara ya mwisho walipokutana na polisi. 

Wananchi wawili kati ya watano (41%) walilipa rushwa hiyo, na wananchi 2% walitoa rushwa wenyewe bila kuombwa. 

Aina ya pili ya rushwa iliyoonekana kutendeka kwa kiasi kikubwa ni wakati wananchi wanatafuta kazi: mtu mmoja kati ya watatu (34%) aliombwa malipo yasiyo rasmi alipokuwa akitafuta kazi.

Hata hivyo, mara nyingi wananchi wana misimamo imara kwenye rushwa; rushwa huombwa mara nyingi sana, lakini wananchi hutoa mara chache tu. 

Mtu 1 kati ya 10 ameripoti kuwahi kutoa rushwa kwa ajili ya kupata kazi.

 Rushwa hutolewa sana kwa polisi, na pia wakati wa kutafuta huduma za afya: wananchi 19% wameripoti kuwahi kuombwa rushwa, na wananchi 15% wameripoti kuwa walitoa rushwa hiyo walipoiombwa.

 Kwa ujumla, wananchi hutoa rushwa mara chache kuliko wanavyoombwa- kunaonekana kuwa kuna msukumo zaidi wa kutoa rushwa wakati wanatafuta huduma muhimu sana kama vile elimu, huduma za afya, maji, na huduma kutoka serikali ya kijiji/mtaa.

Ingawa wananchi hukumbana na rushwa mara kwa mara katika maisha yao ya kila siku, wengi wao hawafahamu ni hatua gani zakuchukua wanapoombwa rushwa.

 Ni mtu mmoja tu kati ya watatu (33%) anayejua kuwa anatakiwa kuripoti vitendo vya rushwa kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). 

Cha kushangaza zaidi, wananchi tisa kati ya kumi (93%) hawajawahi kutoa taarifa za rushwa kwenye mamlaka husika katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Kwa ujumla, wananchi 3 kati ya 4 (76%) wanafikiri kuwa rushwa imekithiri zaidi ndani ya kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Linapokuja suala la rushwa katika ngazi ya taifa, wananchi hawana taarifa za kutosha kuhusu rushwa hizo.

 Kati ya kashfa mbalimbali za rushwa zilizoibuliwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, Watanzania wanne kati ya kumi (37%) hawajawahi kusikia kuhusu kashfa zinazohusiana na IPTL, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (Jairo), Rada ya BAE, EPA au Richmond. 

Kashfa inayojulikana zaidi ni ile ya Richmond; Watanzania zaidi ya nusu (56%) wamewahi kuisikia angalau kidogo, lakini ni Mtanzania 1 tu kati ya 7 (13%) anayeweza kutoa maelezo sahihi kuhusu kashfa hiyo.

Licha ya kukosa uelewa, wananchi 8 kati ya 10 (78%) wanaamini kuwa rushwa imekithiri zaidi ndani ya kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Mbali na kutofahamu ufisadi mkubwa wa fedha za umma, wananchi pia hawana taarifa kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kupambana na rushwa. 

Ni mwananchi 1 tu kati ya 4 anafahamu uwepo wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, na mwananchi 1 tu kati ya 5 anayejua ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

 Hata hivyo, wananchi wanataka Serikali iwajibike zaidi. 

Walipopewa taarifa kuhusu matokeo ya hivi karibuni ya matumizi mabaya ya fedha yaliyoripotiwa kwenye ripoti za CAG, wananchi watatu kati ya wanne wanaamini kuwa watu waliohusika wanapaswa kuwajibishwa kwa upotevu wa fedha za umma.

Kutokana na kushamiri kwa rushwa katika maisha ya kila mtanzania, kukosekana kwa uelewa wa fursa zilizopo kurekebisha au kutatua tatizo ni vyema ijulikane kuwa pengine hii ndiyo sababu ya Watanzania (51%) kufikiri kuwa rushwa haiwezi kupunguzwa kabisa.

Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alisema "Ni jambo la kusikitisha kuwa licha ya juhudi nyingi, wananchi bado wanakumbana na rushwa katika maisha yao ya kila siku na katika sekta zote, hususan kwenye huduma za serikali."

"Na kuhusu suala la rushwa katika ngazi ya taifa," aliendelea, "inaonekana kuwa kuna kuvunjika kwa muafaka wa kijamii na kisiasa kati ya Serikali na wananchi. 

Kwa sasa, wananchi waonekana kuwa hawajui au hawana shauku ya kufuatilia rushwa kubwa kubwa. 

Wanasiasa, NGOs na vyombo vya habari vinapiga kelele kuhusiana na jambo hili, lakini wananchi wa kawaida hawaonekani kuhusisha rushwa kubwa na matarajio yao ya kila siku."

Rajani alisisitiza kuwa, "Matokeo haya ya utafiti yanaonesha kuwa licha ya jitihada za kuboresha utawala na ahadi za mara kwa mara za uwazi serikalini, mambo matatu yanatawala: rushwa imeenea kwenye maisha ya kila siku ya watu wa kawaida; hali ya rushwa inazidi kuwa mbaya; na wananchi hawaamini kuwa serikali au upinzani wanaweza au wataweza kupunguza rushwa.”


Imetolewa leo Agosti 5,2014 na Risha Chande

Communications Manager

Twaweza
Dar es salaam

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post