Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe akisisitiza kuhusu umuhimu wa akina mama kufika katika vituo vya afya pamoja na hospitali-Picha zote na Kadama Malunde-Shinyanga |
Kufuatia takwimu kuonesha kuwa akina mama wengi mkoani Shinyanga wamekuwa wakijifungulia majumbani,akina mama wametakiwa
kubadilika na kuanza kwenda kujifungulia katika vituo vya afya na hospitali
badala kwani wamekuwa wakikosa fursa nyingi za uzazi wa
mpango zinazopatikana maeneo hayo,zinazotolewa na serikali pamoja na mashirika mbalimbali yaliyojitolea kusaidia katika sekta ya afya nchini Tanzania.
Rai hiyo imetolewa leo na mganga mkuu wa
mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya mratibu wa kitengo cha
mawasiliano na utetezi shirika la EGPAF(Elizabeth Glaser Pediatric Aids
Foundation) Mercy Nyanda,shirika linalojihusisha na kutokomeza maambukizi ya
virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto likifadhiliwa na watu wa
Marekani kupitia shirika la USAID na CDC.
Dkt Kapologwe alisema hivi sasa asilimia
35 hadi 40 ya akina mama mkoani Shinyanga wanajifungulia majumbani hali ambayo
inawafanya wakose fursa zinazopatikana katika vituo vya afya na hospitali.
"Hii ni hatari,tunaomba sasa jamii ibadilike,mama mjamzito akifika hospitali ama katika vituo vya afya ataelimishwa kuhusu uzazi wa mpango atapimwa afya yake,na kama ana
maambukizi ya VVU basi kuna huduma zinatolewa ili mtoto asipate maambukizi,pia atapimwa ili
kujua kama ana saratani ya mlango wa kizazi",alieleza Dkt Kapologwe.
Alisema kwa
kushirikiana na EGPAF,na asasi yake ya kiraia inayofanya kazi mkoani Shinyanga iitwayo Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative(AGPAHI) sasa mkoa umefanikiwa kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja vifo vinavyotokana na uzazi.
Aidha aliongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na mashirika hayo wanaamini kuwa ifikapo 2015 mkoa wa Shinyanga utakuwa umefikia asilimia 50
kuwa na vituo vya upasuaji kutoka asilimia
10 iliyopo hivi sasa.
Katika hatua nyingine alilipongeza
shirika la EGPAF na AGPAHI kwa ushirikiano wake katika sekta ya afya hususani katika
mradi wake wa uzazi wa mpango,mradi wa saratani ya mlango wa kizazi sambamba na
kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Aliongeza kuwa EGPAF na AGPAHI wamekuwa mstari wa mbele
kusaidiana na serikali katika kuimarisha afya ya jamii kwa kuwajengea uwezo
wataalam wa afya na kusambaza vifaa tiba katika vituo vya afya na hospitali.
"Kwa kushirikiana EGPAF,na Shirika la AGPAHI tumeweza
kuhamasisha akina mama wengi kufika hospitali mfano katika hospitali hii kila siku tunapokea akina mama 15 hadi
20 kupima afya zao",aliongeza Dkt Kapologwe.
Alisema katika mkoa wa Shinyanga kuna
hospitali 5,vituo vya afya 18 na zahanati 187 huku takwimu zikionesha kuwa
asilimia 12.5 ya wakazi wa mkoa huo wanatumia uzazi wa mpango.
Alizitaja baadhi ya sababu za wananchi kutofuata
uzazi wa mpango kuwa ni mila potofu kwani wengine wanaamini kuwa uzazi wa
mpango unasababisha ugumba na wengine kuamini kuwa na watoto wengi ni fahari sambamba na mtawanyiko
mdogo wa vituo vya kutolea huduma za Uzazi wa Mpango
Naye muuguzi katika kitengo cha uzazi wa
mpango katika hospitali hiyo Elizabeth Sabuni,ambaye ni miongoni mwa wataalam wa afya waliojengewa uwezo na EGPAF alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi wawaeleze
madhara ya ngono katika umri mdogo ili kuepuka vifo visivyokuwa vya lazima.
Naye mratibu wa kitengo cha mawasiliano na
utetezi kutoka EGPAF bi Mercy Nyanda alieleza kufurahishwa namna miradi yake
inavyotekelezwa mkoani Shinyanga katika kutokomeza vifo vya akina mama na
watoto.
Ziara ya siku nne mkoani Shinyanga ya mratibu
wa kitengo cha mawasiliano na utetezi kutoka EGPAF ambaye ameambatana na
waandishi wa habari inalenga kufanya tathmini juu ya utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na shirika
hilo kwa hisani ya watu wa Marekani kupitia shirika la USAID na CD,ambayo ni
kuhusu uzazi wa mpango,uchunguzi kuhusu saratani ya shingo ya kizazi na
kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,ambayo
inatekelezwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga na vito mbalimbali vya afya.
Na Kadama Malunde-Shinyanga