Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAWAKE MKOANI SHINYANGA WATAKIWA KUACHA KUJIFUNGULIA MAJUMBANI

Ndani ya ofisi ya mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe(kushoto) ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya mratibu wa kitengo cha mawasiliano na utetezi shirika la EGPAF(Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation) Mercy Nyanda kutoka Dar es salaam,shirika linalojihusisha na kutokomeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto likifadhiliwa na watu wa Marekani kupitia shirika la USAID na CDC mkoani Shinyanga kufanya tathmini juu ya miradi inayosimamiwa na EGPAF katika hospitali na vituo vya afya

Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe akizungumza na waandishi wa habari walioambatana mratibu wa kitengo cha mawasiliano na utetezi shirika la EGPAF(Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation) Mercy Nyanda katika ziara yake ya siku 4 mkoani Shinyanga iliyoanza Agosti 12,2014
 

Mratibu wa kitengo cha mawasiliano na utetezi shirika la EGPAF(Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation) Mercy Nyanda(mwenye nguo nyekundu) akisikiliza maelezo kutoka kwa mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe kuhusu namna hospitali ya mkoa inavyotekeleza miradi inayosimamiwa na EGPAF kwa hisani ya watu wa Marekani kupitia shirika la USAID na CDC 
Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe akisisitiza kuhusu umuhimu wa akina mama kufika katika vituo vya afya pamoja na hospitali-Picha zote na Kadama Malunde-Shinyanga

Kufuatia takwimu kuonesha kuwa akina mama wengi mkoani Shinyanga wamekuwa wakijifungulia majumbani,akina mama wametakiwa kubadilika na kuanza kwenda kujifungulia katika vituo vya afya na hospitali badala kwani wamekuwa wakikosa fursa nyingi za uzazi wa mpango zinazopatikana maeneo hayo,zinazotolewa na serikali pamoja na mashirika mbalimbali yaliyojitolea kusaidia katika sekta ya afya nchini Tanzania.

Rai hiyo imetolewa leo na mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya mratibu wa kitengo cha mawasiliano na utetezi shirika la EGPAF(Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation) Mercy Nyanda,shirika linalojihusisha na kutokomeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto likifadhiliwa na watu wa Marekani kupitia shirika la USAID na CDC.

Dkt Kapologwe alisema hivi sasa asilimia 35 hadi 40 ya akina mama mkoani Shinyanga wanajifungulia majumbani hali ambayo inawafanya wakose fursa zinazopatikana katika vituo vya afya na hospitali.

"Hii ni hatari,tunaomba sasa jamii ibadilike,mama mjamzito akifika hospitali ama katika vituo vya afya ataelimishwa kuhusu uzazi wa mpango atapimwa afya yake,na kama ana maambukizi ya VVU basi kuna  huduma zinatolewa ili mtoto asipate maambukizi,pia atapimwa ili kujua kama ana saratani ya mlango wa kizazi",alieleza Dkt Kapologwe.

Alisema kwa kushirikiana na EGPAF,na asasi yake ya kiraia inayofanya kazi mkoani Shinyanga iitwayo Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative(AGPAHI) sasa mkoa umefanikiwa kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja vifo vinavyotokana na uzazi.

 Aidha aliongeza kuwa  serikali kwa kushirikiana na mashirika hayo wanaamini kuwa ifikapo 2015 mkoa wa Shinyanga utakuwa umefikia asilimia 50 kuwa na  vituo vya upasuaji kutoka asilimia 10 iliyopo hivi sasa.

Katika hatua nyingine alilipongeza shirika la EGPAF  na AGPAHI kwa ushirikiano wake katika sekta ya afya hususani katika mradi wake wa uzazi wa mpango,mradi wa saratani ya mlango wa kizazi sambamba na kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

 Aliongeza kuwa EGPAF na AGPAHI wamekuwa mstari wa mbele kusaidiana na serikali katika kuimarisha afya ya jamii kwa kuwajengea uwezo wataalam wa afya na kusambaza vifaa tiba katika vituo vya afya na hospitali.

"Kwa kushirikiana EGPAF,na Shirika la AGPAHI tumeweza kuhamasisha akina mama wengi kufika hospitali mfano katika hospitali hii kila siku tunapokea akina mama 15 hadi 20 kupima afya zao",aliongeza Dkt Kapologwe.

Alisema katika mkoa wa Shinyanga kuna hospitali 5,vituo vya afya 18 na zahanati 187 huku takwimu zikionesha kuwa asilimia 12.5 ya wakazi wa mkoa huo wanatumia uzazi wa mpango.

Alizitaja baadhi ya sababu za wananchi kutofuata uzazi wa mpango kuwa ni mila potofu kwani wengine wanaamini kuwa uzazi wa mpango unasababisha ugumba na wengine kuamini kuwa na watoto wengi ni fahari  sambamba na mtawanyiko mdogo wa vituo vya kutolea huduma za Uzazi wa Mpango


 Naye muuguzi katika kitengo cha uzazi wa mpango katika hospitali hiyo Elizabeth Sabuni,ambaye ni miongoni mwa wataalam wa afya waliojengewa uwezo na EGPAF alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi wawaeleze madhara ya ngono katika umri mdogo ili kuepuka vifo visivyokuwa vya lazima.

 Naye mratibu wa kitengo cha mawasiliano na utetezi kutoka EGPAF  bi Mercy Nyanda alieleza kufurahishwa namna miradi yake inavyotekelezwa mkoani Shinyanga katika kutokomeza vifo vya akina mama na watoto.

Ziara ya siku nne mkoani Shinyanga ya mratibu wa kitengo cha mawasiliano na utetezi kutoka EGPAF ambaye ameambatana na waandishi wa habari inalenga kufanya tathmini juu ya  utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na shirika hilo kwa hisani ya watu wa Marekani kupitia shirika la USAID na CD,ambayo ni kuhusu uzazi wa mpango,uchunguzi kuhusu saratani ya shingo ya kizazi na kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,ambayo inatekelezwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga na vito mbalimbali vya afya.

Na Kadama Malunde-Shinyanga


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com