UONGOZI wa Serikali kwenye Tarafa ya Ngaherango, Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, umepiga marufuku wafugaji wa kabila la Wasukuma kwenye tarafa hiyo, kutembea na fimbo mitaani ili kukomesha tabia ya kuchapana ovyo hata kusababisha mauaji.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye vijiji vya Ngoheranga na Ihowanja wilayani humo, Ofisa Tarafa wa Kijiji cha Ngoheranga, Conrad Mzwalandili, alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya matumizi mabaya ya fimbo hizo.
Katika mkutano huo, wananchi walitaka kujua sababu za uongozi wa Serikali katika tarafa hiyo kutoa agizo hilo wakati wafugaji wa kabila hilo ni utamaduni wao kutembea na fimbo.
Mzwalandili alisema, imebainika baadhi ya vijana ambao hutembea na fimbo, huchapana hata kusababisha mauaji na tayari zaidi ya fimbo sabini zimekamatwa akiwataka wakazi wa eneo hilo kutembea kwa kujiamini kwani Tanzania ni nchi huru.
Mbali ya agizo hilo, pia alisema wamepiga marufuku ngoma aina ya chagulaga ambayo imekuwa ikiwadhalilisha mabinti wakiwemo wanafunzi ambapo vijana zaidi ya 100, humkimbiza binti bila kujali ni mwanafunzi au vinginevyo na kumfanyia vitendo visivyofaa.
“Kama ni tamaduni zenu, fanyieni nyumbani kwenu tena ndani na si barabarani...yeyote ambaye atakwenda kinyume na agizo hili atachukuliwa hatua,” alisema Mzwalandili na kusisitiza Kamati ya Ulinzi na Usalama imeridhia kupigwa marufuku ngoma hiyo, kutembea na fimbo.
via>>Majira
Social Plugin