VIONGOZI Wakuu wa Vyama vya siasa vyenye Wabunge vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wamekuwa katika mashauriano ya zaidi ya mwezi mmoja tangu tarehe 2 Agosti mwaka huu huku wakishauriana juu ya mwenendo wa mchakato wa Katiba Mpya na jinsi ya kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki hapo mwakani.
Akiongea kwa niaba ya viongozi wengine wa kituo hicho, Mhe. John Cheyo amesema kuwa Katika mashauriano hayo yaliyochukua sura ya Kamati ya Makatibu Wakuu, Kamati ya Wenyeviti wa Vyama vya CCM, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi katika hatua tofauti. Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kamati zote zilitoa taarifa zao kwenye vikao vya Viongozi Wakuu wa Vyama (Summit) ya TCD ambayo wajumbe wake ni Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa Vyama wanachama.
Mhe. Cheyo aliongeza kuwa katika kutafuta maridhiano, Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa Vyama walifanya mashauriano na Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete siku ya Agosti 31 na tena Nane Septemba 8, 2014 hapa Ikulu ndogo mjini Dodoma.
“Pamoja na kazi ya msingi inayofanywa na Bunge Maalum la Katiba, mchakato wa Katiba unaoendelea sasa hauwezi kutupa Katiba itakayotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuwa muda hautoshi kukamilisha mchakato na kufanya mabadiliko yatakayohitajika ya Sheria, Kanuni na Taasisi mbalimbali zitakazohitajika”, alisema Mhe. Cheyo.
Mhe. Cheyo aliendelea kwa kusema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwisho wa mchakato ni kura ya maoni itakayofanyika mwezi Aprili 2015. “Kama itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa Sheria iliyotajwa, kura itarudiwa mwezi Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa livunjwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2015 na ili Katiba Mpya itumike katika uchaguzi Mkuu utakaokuja, itabidi uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo hatuliungi mkono”, alisisitiza Mhe. Cheyo.
Mhe. Cheyo amesema kuwa Bunge Maalum la Katiba kwa sasa linafanya kazi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na 254 lililotolewa na Mhe. Rais Kikwete tarehe 1 Agosti, 2014. “Tangazo hilo litatumika hadi tarehe 4 Oktoba, 2014 ambapo Katiba inayopendekezwa inategemewa kupatikana, Wajumbe walikubaliana hatua hii iachwe ifikiwe”, alisema Mhe. Cheyo.
Kuhusiana na Kura ya maoni, Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Bunge hilo kumaliza kutunga Katiba, ingefuata hatua ya kura maoni kuthibitisha Katiba. “Kwa kutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015 kuahirishwa, basi hatua hii iahilishwe, na mchakato wa Katiba uendelee baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015”, alisema Mhe. Cheyo.
Sambamba na hayo, Mhe. Cheyo ameishauri Serikali kuchukua hatua za kisheria ili matayarisho kwa ajili ya Uchaguzi wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa, yaanze haraka iwezekanavyo ili uchaguzi ufanyike mapema hapo mwakani. Aidha, amegusia kuhusu Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 akasema kuwa, kwa vile Uchaguzi Mkuu wa 2015 utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, kuna umuhimu kufanya mabadiliko kidogo (minimum reforms) katika Katiba pamoja na sheria ya Uchaguzi yatayowezesha nchi kufanya uchaguzi huru na wa haki.
“Tayari mambo yafuatayo yamekubaliwa, kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kusimam
ia uchaguzi, Mshindi wa Uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50% (50%+1)”, alisema Mhe. Cheyo. Viongozi hao Wakuu wa Vyama wamempongeza Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa ujasiri wake na imani yake katika kuimarisha demokrasia nchini na kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya nchi.
“Tunampongeza kwa kukubali kukutana na kushauriana nasi kuhusu mambo ya muhimu kwa mustakabali wa taifa letu kwa lengo la kudumisha amani, upendo na mshikamano ili nchi yetu iende kwenye uchaguzi ikiwa ni nchi ya kujivunia yenye amani, mshikamano na itakayokuwa na Uchaguzi Huru na wa haki, lakini pia tunajipongeza sisi wenyewe Wakuu wa Vyama kwa kuwa tumetoka mbali na misimamo yetu, lakini utaifa umetufanya tukubaliane katika mambo ya msingi wa Taifa letu”, alipongeza Mhe. Cheyo
via>mwanaharakatimzalendo blog
TUNAPENDA TUKUTUMIE HABARI ZETU MARA TU ZINAPOTOKEA, LIKE PAGE YETU SASA HIVI UENDE NA WAKATI. BONYEZA HAYA MANENO
TUNAPENDA TUKUTUMIE HABARI ZETU MARA TU ZINAPOTOKEA, LIKE PAGE YETU SASA HIVI UENDE NA WAKATI. BONYEZA HAYA MANENO
Social Plugin