KIJANA HUYU AUAWA KWA KUCHOMWA VITU KICHWANI NA KIFUANI AKITUHUMIWA KUWAROGA WATOTO NA KUTUMIKISHA WATU KICHAWI

Marehemu Gabriel Mwandemwa(Mwasyebule) enzi za uhai wake, Marehemu alikuwa akijishughulisha na biashara mbali mbali ikiwemo uuzaji wa maziwa na ununuzi wa mahindi.

Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi bado yanazidi kuyakumba baadhi ya maeneo mkoani Mbeya ambapo katika tukio la jana  kijana  wa miaka 39 ameuawa na wananchi wenye hasira kali wakimtuhumu kwa imani za kishirikina.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kumtaja marehemu kuwa ni Gabriel Mwandemwa (Mwasyebule) mkazi wa kijiji cha Ikamambande Wilaya ya Rungwe.

Alisema  kijana huyo aliuawa na watu wasiofahamika kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali sehemu za kichwani na kifuani.

Alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa tano asubuhi huko katika Kijiji cha Ikamambande, kata ya Lwangwa, Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.

Alisema taarifa za awali zinadaiwa kuwa, uongozi wa kimila kijijini hapo  uliitisha kikao cha dharura ukihusisha viongozi wa vitongoji na vijiji jirani na ndipo waliamua kumtafuta na kumlazimisha marehemu kuhudhuria katika kikao hicho na kisha kuanza kumpiga na kupelekea kifo chake.

Alisema marehemu alikuwa akituhumiwa kuwa ni mshirikina kijijini hapo kwa kuwa anawaroga watoto na kuwa anajipatia mazao mengi kwa kuwatumikisha watu kishirikina.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post